Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima waonyeshwa fursa miti ya mitiki

Mitiki Miti ya Mitiki

Wed, 15 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

IMEELEZWA kuwa hekari moja ya miti aina ya mitiki inaweza kumwingizia mkulima zaidi ya Sh. milioni 400 na kujiletea manufaa ya kujiimarisha kiuchumi.

Hayo yalisemwa na Ofisa wa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Bagingo Bugingo, alipokuwa akizungumza na wanahabari na wakulima wanaotekeleza mradi wa kupanda miti kibiashara.

Hamasa hiyo inatokana na halmashauri hiyo kuweka lengo la kupanda miti hekari 1,750.

Bugingo alisema kuwa katika harakati za kufika malengo hayo, hadi sasa wilaya hiyo imeshapanda miti katika eneo la hekari 317.5 na miti yote inaendelea vizuri.

Alisema hata hivyo, wakulima wengi katika mwambao mwa Ziwa Nyasa wanakata tamaa ya kuendelea kupanda miti hiyo ambayo tangu kupandwa hadi kuvunwa inachukua kati ya miaka 15 hadi 20.

Alisema mradi wa pandamiti kibiashara unatekelezwa katika safu ya Milima ya Livingstone katika kata za Lipingo, Liuli, na Kihagara Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na kwamba unaendelea kwa kiwango cha kuridhisha.

Naye Mratibu wa Mradi wa Forvac Mkoa wa Ruvuma, Marcel Mtunda, akikagua mradi wa panda miti kibiashara unaotekelezwa katika Kijiji cha Mkali ‘A’ na Kijiji cha Nkalachi Kata ya Liuli, na kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ukuaji wa miti, na kuwaomba wananchi wapalilie miti hiyo ili isiungue kwa moto.

Alisema wananchi baada ya kupata elimu ya upandaji miti kibiashara, wamehamasika na kupanda miti ambapo amesema mradi huo utawanufaisha wakulima wa miti katika vijiji hivyo kwa kuinua hali ya maisha na kuongeza kipato katika ngazi ya familia.

Rais wa Shirikisho la Viwanja vya Misitu Tanzania (SHIVIMITA), Ben Mfungo, alisema tangu mwaka 1988 mahitaji ya soko la miti aina ya mitiki limekuwa likiendelea kukua ndani na nje ya nchi.

“Juzi tu nilikuwa Accra nchini Ghana, tulijulishwa kwamba Jumuiya ya ECOWAS ilichukua mbegu za miti ya mitiki toka Tanzania baada ya kubainika mbegu za Tanzania zina ubora zaidi katika soko la dunia, hivyo nao wameamua kuchukua mbegu hiyo inayokidhi soko la kimataifa,” alisema Mfungo.

Kufutia hali hiyo aliwataka wakulima wapya wa mitiki katika Wilaya ya Nyasa na maeneo mengine ambayo zao hilo linaweza kustawi, waongeze uzalishaji wa mitiki kwa sababu mahitaji yake yanaendelea kuongezeka.

“Mahitaji ya mti huu katika soko la duniani ni makubwa, ndiyo maana nchi za Ulaya na za Asia zikiongozwa na China na India wananunua miti aina ya mitiki kwa wingi kutoka Tanzania na hatujaweza kufikisha hata robo ya mahitaji yao,” alibainisha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wiaya ya Nyasa, Jimson Mhagama, aliwashauri wananchi na kampuni za wawekezaji wanaohitaji kuwekeza katika sekta ya misitu wafikie katika wilayani Nyasa kuwekeza kwenye ardhi yenye rutuba.

Mshauri wa Misitu katika Mradi wa Panda Miti Kibiashara, Sangito Sumari, alisema katika Wilaya ya Nyasa mradi huu unahusu miti aina ya mitiki ambayo utafiti umebaini inastawi vizuri katika hali ya hewa iliyopo mwambao mwa Ziwa Nyasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live