Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wanavyonufaika  mradi wa kilimo cha mpunga

5007809d7b1ea30f4d388a327c7fe8b4 Wakulima wanavyonufaika  mradi wa kilimo cha mpunga

Tue, 27 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUMEKUWEPO na jitihada mbalimbali za kuwawezesha wakulima hususani wa mpunga kulima kisasa zaidi ili kuongeza uzalishaji, chakula na kipato.

Jitihada hizo zinaleta matumaini kwa mkulima hususani katika miaka hii yenye changamoto mbalimbali za kilimo kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Hatua za kulima kisasa kunakowahakikishia mavuno ya kutosha, kunarudisha matumaini kwa wakulima kwani sasa wanawezesha kuvuna zaidi tofauti na ilivyokuwa awali.

Semeni Abdallah (30) ni miongoni mwa wakulima 1,600 wanaoshiriki kwenye utekelezaji wa mradi wa kutengeneza mnyororo wa thamani endelevu na shindani wa zao la mpunga unaotekelezwa na Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero iliyopo mkoani Morogoro.

Ushuhuda wa Semeni ni kwamba mradi huo umeweza kumwongezea uzalishaji, chakula cha kutosha na kipato.

Anasema kabla ya mradi huo kuanza, yeye pamoja na wakulima wenzake wanaolima mpunga kwenye skimu ya Mkindo walikuwa wanazalisha gunia 10 hadi 15 tu za mpunga kwenye eka moja.

Lakini msimu uliopita baada ya mradi huo kuwawezesha kuendesha kilimo cha mpunga cha kisasa wameweza kuvuna magunia 40 ya mpunga kwenye eka ile ile moja.

“Mafanikio haya yametokana na mradi kutuwezesha kwenye mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutupatia mafunzo ya Kilimo Shadidi ambacho kinatumia mbegu kidogo, mbolea kidogo na kufuata kwa umakini kanuni bora za kilimo.

“Kutuunganisha na watoa huduma kama vile wasambazaji wa pembejeo na kutuwezesha kupata mbegu na mbolea bora kwa bei nafuu na kwa wakati, kutuunganisha na watoa huduma ya zana za kilimo kwa ajili ya kuandaa mashamba na kuvuna mpunga, kutuunganisha na vyombo vya fedha kwa ajili ya kupata mikopo ya pembejeo na kilimo,” anasema.

Mkulima mwingine, Shaban Magana (40) anakiri mradi huo umewaongezea uzalishaji katika zao la mpunga na kupunguza gharama za uzalishaji.

Hata hivyo anasema miundombinu mibovu kwenye skimu bado ni changamoto inayopunguza utendaji wao. Anataja pia barabara kwamba zinasababisha usafirishaji wa mavuno kuwa mgumu.

“Inamgharimu mtu Sh 10,000 kusafirisha gunia moja la mpunga kutoka shambani hadi kwenye ghala kutokana na ubovu wa barabara. Hii ni gharama kubwa sana kwa mkulima,”.

Anasema bei ya mpunga kuwa chini ni changamoto nyingine inayokwamisha jitihada hizo za wakulima kwani kwa sasa gunia la mpunga linauzwa kati ya Sh 40,000 hadi 50,000 ikilinganishwa na Sh 100,000 kwa misimu miwili iliyopita.

“Tatizo la Corona nalo limetuathiri kwa kiasi kikubwa kwani wanunuzi kutoka nchi jirani kama Kenya hawaji tena kununua mazao yetu kutokana na zuio la kusafiri,” anasema.

Kwa upande wake, Mtaalamu Elekezi wa Mradi huo, Hendry Mziray anasema lengo maalumu la mradi huo ni kuwawezesha wakulima wadogo hususani wanawake na vijana kutengeneza mnyororo wa thamani shindani na endelevu wa zao la mpunga ili kuongeza uzalishaji, usalama wa chakula na kuongeza kipato katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi.

Mziray anasema mradi huo unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo (IFAD) na Mtandao wa Vyama wa Wakulima Kusini mwa Bara la Africa (SACAU).

Anasema watekelezaji wa mradi ni Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) kwa kuwashirikisha wadu mbalimbali wa sekta za umma na binafsi.

“Mradi huu unatumia mfumo wa mnyororo wa thamani na ubia wa sekta binafsi na umma, unalenga kuwafikia wakulima 1,600 kwenye skimu za Dakawa na Mikindo wengi wao wakiwa ni wanawake na vijana.

“Kwa mwaka mmoja sasa tumeanza kuona matokeo chanya ya mradi, kwani wakulima wameweza kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa gunia 15 hadi 20 na kufikia kati ya gunia 35 hadi 40 za mpunga kwenye eka moja,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa ACT, Timoth Mmbaga, anasema baraza hilo ni chombo kilele cha wadau wa sekta binafsi wanajishughulisha na masuala ya kilimo, mifugo, uvuvi na mengineyo.

Mmbaga anaelezea kazi ya ACT kuwa ni utetezi na ushawishi ili kutengeneza mazingira wezeshi ya kibiashara na uwekezaji wa sekta binafsi kwenye kilimo na kufanya sekta hii muhimu kukua na kutoa mchango mkubwa kwenye kujenga uchumi wa taifa.

Anasema baraza hilo pia linawajengea uwezo wanachama wake hususani wakulima wadogo ili waweze kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na chenye manufaa kwa wazalishaji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz