Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima walipwa Sh374 milioni kufidia athari ya mvua

Fedhaa 0 Wakulima walipwa Sh374 milioni kufidia athari ya mvua

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima 1,398 wa zao la tumbaku wamelipwa zaidi ya Sh374 milioni kufidia hasara waliyopata baada ya mazao yao kuharibiwa na mvua ya mawe shambani.

Hundi ya malipo hayo kwa wakulima kutoka Wilaya za Sikonge, Kaliua na Urambo imekabidhiwa leo Oktoba 25, 2023 baada ya kukata bima ya mazao kupitia Benki ya NMB.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa hundi hiyo, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima (TIRA) Kanda ya Magharibi, Emmanuel Lupilya amewasihi wakulima wengine kuiga mfano wa wenzao kwa kukata bima ya mazao yao ili wanufaike kwa kufidiwa majanga yanapotokea.

"Tukumbuke majanga ya mvua ya mawe, ukame na mengine ya aina hiyo yanatokea bila kutarajiwa; ni vema kila mkulima ahakikishe anakata bima ya mazao kwa tahadhari ya uharibifu wowote. Tujifunze kutoka kwa hawa wakulima wanapokea fidia ya mazao yao yaliyoharibiwa na mvua yam awe,’’ amesema Lupilya

Meneja huyo aliyemwakilisha Kamishna wa TIRA, Dk Abdallah Sakware, amewahakikishia wakulima wanaokata bima kuwa mamlaka hiyo itasimamia na kufanikisha malipo ya fidia kama ilivyofanya kwa wakulima wa tumbaku waliokuwa wanapokea hundi zao za malipo ya fidia.

Akikabidhi hundi hiyo kwa wawakilishi wa wakulima waliohudhuria hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amewapongeza wakulima waliokatia bima mazao yao huku akiwahimiza wengine kuiga mfano huo.

Amewataka wakulima wa mazao yote mkoani humo kuchukua tahadhari kwa kukatia bima mazao yao, hasa katika kipindi hiki ambacho Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari ya mvua za El Nino.

‘’Kama wapo wakulima waliokuwa na mashaka kuhusu fidia ya uharibifu wa mazao sasa wajifunze kupitia kwa wenzao wanaolipwa fidia kwa sababu wamejionea wenyewe malipo yakifanyika,’’ amesema Dk Burian

Mkuu wa Idara ya Kilimo na Biashara Benki ya NMB, Nsolo Mlozi amewahakikishia wakulima kote nchini kuwa benki hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine ikiwemo TIRA itaendelea kutoa elimu kwa wakulima na makundi mengine ya kijamii kuhusu umuhimu wa bima ya mazao ili kupata fidia ya hasara inayotokana na majanga.

"Malipo ya fidia itawasaidia wakulima siyo tu kupunguza hasara, bali pia itawaongezea ari na nguvu mpya katika maandalizi ya msimu mwingine wa kilimo,’’ amesema Mlozi

Chanzo: www.tanzaniaweb.live