Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima walilia soko la mchele nje ya nchi

17861 Mchele+pic TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wakulima wa mpunga nchini wameiomba Serikali kuondoa zuio la usafirishaji wa mchele nje ya nchi kutokana na kiasi kilichopo sasa cha ziada ya tani 1.2 milioni kukosa soko la uhakika la ndani.

Wakulima hao wakizungumza na Mwananchi jana mjini Moshi baada ya kumalizika kwa semina iliyoandaliwa na Bodi ya Mpunga kwa wakulima wa zao hilo kutoka mikoa inayolima zao hilo, walisema shida yao ni masoko.

Walisema kukosekana kwa soko la uhakika kumefanya bei ya mchele kudorora na kuwasababishia hasara kwa sababu wanatumia gharama kubwa katika uzalishaji wake.

Halima Faraji, mkulima wa mpunga kutoka mkoani Morogoro alisema wanamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa asikie kilio chao kwa sababu hivi sasa wanazalisha zao hilo kwa wingi.

Mkulima wa zao hilo, George Masenene kutoka mkoani Mbeya, alisema Serikali inasisitiza walime mazao ya kutosha, lakini haiwapatii mbadala wa soko la uhakika, hali inayozidi kuwatengenezea changamoto wakulima wengi kiasi cha kukata tamaa.

“Serikali inatushauri tuzalishe mpunga kwa wingi, lakini cha kushangaza masoko hakuna, tunaiomba itupatie kibali cha kuuza bidhaa zetu nje ya nchi ili tuweze kupata faida ya kilimo tunachofanya,” alisema Masenene.

Septemba 12, Serikali ilitoa agizo la kusitisha uagizwaji wa mchele kutoka nje ya nchi kutokana na uliopo nchini kutosheleza mahitaji.

Ilisema mchele uliopo nchini kwa sasa ni tani milioni 2.2, kiwango kilichotokana na wakulima wa mpunga kupatiwa mbinu bora za kitaalamu.

Katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe alisema mahitaji ya nchi kwa sasa ni tani 900,000 na kwamba, uzalishaji umeongezeka na nchi ina ziada ya tani milioni 1.2.

Kenya yazuia mchele

Wakati wakulima wa mpunga wakiomba kuuza zao hilo nje ya nchi, hivi karibuni Serikali ilisema Kenya imezuia uingizaji wa mchele kutoka Tanzania, jambo ambalo linaashiria mvutano wa kibiashara miongoni mwa mataifa hayo mawili.

Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Adolph Mkenda aliliambia gazeti dada la Mwananchi la The Citizen kuwa chanzo cha zuio hilo ni ubora wa mchele na namna unavyofungashwa.

“Bado tunatafuta taarifa zaidi kuhusu zuio hilo lakini nina imani kubwa haya ni mambo yanayozungumzika,” alisema Profesa Mkenda.

Chanzo: mwananchi.co.tz