Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wakatilia pamba yao hadi walipwe

65156 Pamba+pic

Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza/Bariadi. Anguko la bei ya pamba kutoka senti 77 ya dola ya Kimarekani hadi kati ya senti 65 hadi 67 ya dola imeanza kuathiri ununuzi wa zao hilo kwa bei elekezi ya Sh1, 200 kutokana na wanunuzi kuhofia kupata hasara.

Ingawa haijatangazwa rasmi, kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia inadaiwa ni matokeo ya mgogoro wa kibiashara kati ya China ambao ndio wanunuzi wakuu wa pamba na wamiliki wa viwanda vingi vya nguo duniani na Marekani ambao ndio wanunuzi wakuu wa nguo kutoka viwanda vya China.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), Marco Mtunga, inakadiriwa kuwa kila Mmarekani mmoja anavaa nguo zinazotokana na kilo 21 za pamba kila mwaka kulinganisha na kiwango cha kilo tatu kwenye nchi zinazoendelea, zikiwemo za Kiafrika.

Hofu ya hasara miongoni mwa wanunuzi umekwamisha malipo kwa wakulima ambao pamba yao imekusanywa katika maghala ya vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) miezi miwili iliyopita.

Baada ya kusubiri malipo kwa muda mrefu bila mafanikio, wakulima katika baadhi ya maeneo mkoani Simiyu na wamezuia magari ya wanunuzi kusomba pamba kutoka maghala ya Amcos hadi walipwe fedha zao kwa bei elekezi ya Sh1, 200.

Miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na kadhia ya pamba kuzuiwa ghalani ni pamoja na Sapiwi na Nyakabindi wilayani Bariadi.

Pia Soma

Akizungumza na Mwananchi jana, mkulima Maduhu Peter alisema; “Hatutaruhusu gari yoyote kusomba pamba kutoka Amcos hadi tulipwe. Hatuko tayari kukumbwa na yaliyotokea kwa wenzetu (wakulima) wa korosho kule mikoa ya Kusini,”

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na mkulima mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jerome Shija aliyeongeza kuwa baadhi ya wakulima wameanza kuuza pamba yao kimagendo kwa bei ya chini hadi Sh800 kwa kilo kutokana na kubanwa na mahitaji ya kifamilia ikiwemo chakula na gharama za elimu ya watoto wao.

Msimu wa ununuzi wa pamba ulizinduliwa Mei 2, 2019 katika hafla iliyofanyika kijiji cha Kasekese wilaya ya Tanganyika mkoani katavi ambapo Serikali ilitangaza bei elekezi kuwa ni Sh1, 200 kwa kilo moja.

Akizungumzia zuio hilo la wakulima, mmoja wa wanunuzi wa pamba mkoani Simiyu, Jeremia Malongo alisema wanunuzi wanahofia kununua pamba kwa bei elekezi ya Sh1, 200 wakati bei ya zao hilo imeshuka katika soko la dunia hadi kufikia dola 63 za Kimarekani, sawa na Sh800 kwa kilo.

“Tupo tayari kunua pamba yote ya wakulima kwa bei elekezi; lakini Serikali ituhakikishie aidha fidia ya hasara itakayotokana na kushuka kwa bei katika soko la dunia au iwe (Serikali) tayari kunua malobota yote ya pamba tutakayonunua na kubaki kwa kukosa soko,’’ Malongo

Mkoani Simiyu tayari uongozi wa mkoa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka umeitisha kikao cha wadau wa pamba kutafuta muafaka ambapo miongoni mwa makubaliana yaliyofikiwa ni kuondolewa kwa baadhi ya tozo na ushuru kwa wanunuzi.

Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba, Bozi Ogola alisema muafaka huo utafanikisha ununuzi wa pamba kuendelea huku akiahidi kuwa chama hicho kitafuatilia kwa karibu shughuli zote zinazoendelea katika vituo vya ununuzi kubaini changamoto na kuyatafutia ufumbuzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz