Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima waiomba Serikali kutoa ruzuku zao la ufuta Lindi

Ufuta Pc Data Wakulima waiomba Serikali kutoa ruzuku zao la ufuta Lindi

Mon, 7 Aug 2023 Chanzo: Mwananchi

Wakulima mkoani Lindi wameiomba Serikali kuwasaidia ruzuku ya pembejeo katika zao la ufuta ili waweze kumudu gharama za viuatilifu hivyo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.

Baadhi ya wakulima wa zao la ufuta, Mwajuma Seifu na Abdallah Juma wanaoishi katika Kijiji cha Zinga Kibaoni, Halmashauri ya Kilwa mkoani Lindi wamesema Serikali inatoa pembejeo kwenye zao la korosho pekee iangalie na zao la ufuta ili wa mkulima wa zao hilo aweze kupata pembejeo itakayosaidia kupata ufuta uliobora zaidi.

"Zao la ufuta halina pembejeo sisi wakulima wa Zinga tunategemea zao la ufuta na zao hili, huku kwetu linastawi sasa Serikali ifanye jitihada ya kuangalia zao la ufuta kwani zao hili linaongeza pato la mkulima pamoja na Taifa kiujumla," amesema Mwajuma.

Katibu Msaidizi wa Amcos ya Zinga, Ally Shomary amesema changamoto kubwa waliyonayo kama Amcos ni wakulima kutopeleka ufuta wao ghalani hadi wafuatwe majumbani hali inayosababisha ufuta kuchelewa kumalizika kwa wakati.

"Nilienda kwa mkulima mmoja akiwa na gunia ishirini na mwingine gunia hamsini wote hao ufuta waliuweka ndani na kushindwa kuusafirisha hadi ghalani ikabidi mimi na mwenyekiti wangu tuchukue na kuusafirisha kwa gharama zetu. Hiyo ni changamoto kubwa ambayo sisi kama viongozi wa Amcos tunakutana nazo," amesema Shomary.

Mhasibu Mkuu wa Chama Kikuu cha Lindi Mwambao kinachojumuisha wilaya tatu za Lindi Manispaa, Halmashauri ya Kilwa pamoja na Halmashauri ya Mtama, Mabruk Ismail amesema kuwa msimu huu wa 2022/ 2023 changamoto kubwa waliyokutana nayo ni kukosa pembejeo ya zao la ufuta na kuiomba Serikali kuwasaidia wakulima kwenye suala la pembejeo.

"Licha ya pembejeo kukosekana lakini chama changu cha Lindi mwambao kimeweza kupata zaidi ya Sh100 bilioni ya zao la ufuta kwa msimu huu,” amesema.

Hata hivyo, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi, Cecilia Sostenes amesema kuwa mkoa huo umepata kiasi cha Sh193 bilioni katika zao la ufuta na kuwataka wakulima kutumia fedha hizo vizuri walizopata kwenye ufuta kwa kuboresha makazi yao na kupeleka watoto shuleni.

"Sasa hivi tunajiandaa na msimu wa mbaazi tunaishukuru serikali kwa kukubali mfumo wa stakabadhi ghalani hii itasaidia kumkomboa mkulima pia amewataka wakulima kupeleka mbaazi kwenye maghala kwa ajili ya kuanza minada juma lijalo," amesema.

Jumla ya tani 900 ziliuzwa kwenye mnada wa 9 wa Chama Kikuu cha Lindi Mwambao na bei ya juu ikiwa Sh4,062 huku bei ya chini ikiwa Sh4,060.

Chanzo: Mwananchi