Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wagomea bei ya choroko wadai inawadidimiza

Chorokooooo.jpeg Wakulima wagomea bei ya choroko wadai inawadidimiza

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima wa choroko wilayani Kwimba Mkoa wa Mwanza wamekataa na kuipinga bei mpya ya stakabadhi ghalani ya Sh890 kwa kilo ya zao hilo, huku wakiiomba Serikali kuingilia kati kwa kutafuta mnunuzi mwenye bei yenye tija kwao.

Kulingana na bei ya mnada uliotakiwa kufanyika jana Februari 19, 2024 kwa njia ya mtandao katika ukurasa wa Online Trading System (TMX), kilo ya choroko inauzwa Sh890 ikilinganishwa na Sh1,200 iliyouzwa mwaka jana, huku wakidai ahadi ya Serikali ilikuwa kilo moja ingeuzwa kwa zaidi ya Sh1,000.

Mnada wa choroko wilayani Kwimba ulikuwa ufanyike Kata ya Hungumalwa, lakini haukufanyika baada ya wakulima kugoma.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Februari 20, 2024, mkulima wa choroko kutoka Kijiji cha Nyaniga, Kata ya Mwakilyambiti, Abel John amesema kabla msimu mpya wa ununuzi wa zao hilo haujafunguliwa, kilo ya choroko sokoni ilikuwa kati ya Sh1,000 hadi Sh1,100.

Amesema kitendo cha mnunuzi kushusha bei hakikubaliki, hivyo ameiomba Serikali kutafuta mnunuzi mwingine mwenye uwezo wa kununua kwa angalau Sh1,500 kwa kilo kama ilivyoahidiwa.

"Kwa kweli bei ambayo imefikiwa hatujakubaliana nayo kwa sababu huku wafanyabiashara wanakusanya kutoka kwa wakulima wa choroko kwa Sh1,000 na sisi tuliamua kuungana na Chama cha Ushirika cha Mazao, Kilimo na Masoko (Amcos) kwa sababu tuliambiwa watakuwa na bei nzuri, sasa imetoka bei ya Sh890 ambayo hatujaridhika nayo na tulikuwa tunatarajia itauzwa angalau Sh1,500 ili wote tufaidike, lakini imeshuka," amesema John.

Kilio cha John hakitofautiani na cha Lukas Shudu, mkulima wa kutoka Kijiji cha Nyaniga, Kata ya Mwakilyambiti anayedai bei hiyo inalenga kuwakatisha tamaa wakulima kutoendelea na kilimo cha zao hilo ambalo awali waliamini ni mkombozi kwao kiuchumi.

"Mpaka sasa huu mzigo wa choroko naomba usiuzwe, watutafutie soko lingine, si kwamba mkulima akandamizwe tunataka tuuze kuanzia Sh1,500 ili angalau na sisi tufaidike na nguvu zetu," amesema Lukas.

Mwenyekiti afunguka

Mwenyekiti wa Amcos iliyopo Kijiji cha Buhungo Kata ya Hungumalwa wilayani humo, Samson Kadaso amewataka wakulima kutouza choroko iwapo hawaridhishwi na bei iliyotangazwa, huku akisema anaamini Serikali itasaka mwarobaini wa suala hilo.

"Leo bei haikuwaridhisha, kwa hiyo naona tuwe na subira mpaka pale bei itakapokuwa nzuri, ili mkulima anufaike," amesema Kadaso.

Mwenyekiti wa kampuni la Tanyusa inayoendesha Mfumo wa Stakabadhi Ghalani Mkoa wa Mwanza, Malki Mohamedi mbali na kukiri bei hiyo kutokuwa rafiki kwa wakulima, ameiomba Serikali kushughulikia changamoto hiyo mapema ili kuepusha hasara kwa wakulima hao kutokana na mazao hayo kukaa muda mrefu ghalani.

"Mpaka sasa tumekusanya tani 55 na kilo 669 za choroko ambazo zipo ndani, lakini ukiangalia huko nje zipo nyingi, wakulima wanatamani kuleta lakini walikuwa wanasubiri walau waone bei yenye tija waweze kuleta kwa kasi," amesema.

Naye Meneja Viwanda Chama cha Kikuu cha Ushirika Nyanza, Elisha Madamo amesema ili kuepuka hasara kwao na kwa mkulima watasimamisha ukusanyaji wa choroko mpaka pale bei nzuri zitakapotangazwa.

"Wakulima katika kipindi hiki wawe na subira lengo letu ni kuinua kipato cha mkulima na waweze kunufaika kupitia kilimo cha choroko," amesema Madamo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live