Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima, wafanyabiashara kicheko bei ya vitunguu ikipanda

Vitunguu Wakulima, wafanyabiashara kicheko bei ya vitunguu ikipanda

Mon, 7 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bei ya vitunguu imepanda kutoka Sh120,000 kufikia kati ya Sh240,000 hadi Sh260,000 kwa gunia moja huku debe ya zao hilo ikiuzwa Sh45,000 kutoka Sh20,000.

Chombo cha lita tano cha vitunguu kinauzwa Sh10,000 kutoka Sh5,000 wakati mwaka jana kipindi kama hiki kiliuzwa kati ya Sh2,000 hadi Sh3,000.

Akizungumza katika maonesho ya Nane nane ya kanda ya magharibi yenye mikoa ya Tabora na Kigoma Agosti 5, 2023 mfanyabiashara wa vitunguu soko kuu la Tabora, Adam Samson amesema kipindi hiki bei hupanda lakini kwa mwaka huu bei imekuwa ni nzuri zaidi kwao ikilinganisha na miaka ya nyuma kwani imepanda zaidi ya mara mbili.

"Kipindi hiki hata walaji wenyewe wanafahamu kuwa bei inapanda ingawa kwa mwaka huu bei imekuwa kubwa zaidi," amesema

Mkulima wa vitunguu kata ya Puge vinapolimwa kwa wingi, Aidan Nguvumali ameshukuru kupanda kwa bei zaidi mwaka huu akisema yeye na wakulima wenzake watanufaika na kujiinua kiuchumi na hivyo kupambana na umaskini.

Kutokana na bei ya vitunguu kuwa juu Ofisa Kilimo Kampuni ya East-West Seed inayozalisha mbegu na vitunguu vya Mars F1, Alpha Deogratias ameeleza kuwa hiyo ni fursa nzuri kwa wakulima kulima vitunguu, kuingiza kipato kikubwa na kunufaika na kilimo hicho hasa kwa kutumia mbegu za Mars F1 anazosema zinahimili ukame na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya fungus.

Ametoa sifa nyingine ya vitunguu vya mbegu hiyo kuwa ni kuweza kuhifadhiwa kwa miezi sita tofauti na vingine ambavyo huchukua wiki moja kuharibika ambapo ekari moja hutoa gunia 80 hadi 120 na hukomaa baada ya siku 90 hadi 100.

"Hii ni fursa ikitumiwa vizuri na wakulima watanufaika kwa kutumia mbegu zetu ambazo ni bora na tukiwa tunatoa huduma za ugani bure ,"amesema

Deogratias amesema mbegu hiyo inalimwa maeneo yenye ukame na joto huku gharama za uzalishaji kwa ekari zikiwa kati ya Sh1 milioni hadi Sh2 milioni ambapo mkulima halazimiki kuuza kwa hasara kwa kuogopa vitunguu vyake kuharibika ndani ya wiki moja kama vingine.

Ametoa mfano wa debe moja kuuzwa Sh 30,000 na hivyo gunia kufika Sh180,000 kutamfanya mkulima apate Sh14.4 milioni hadi Sh21.6 milioni kwa ekari moja pekee na hivyo kupata faida ya kati ya Sh12 milioni hadi Sh19 milioni.

Meneja mafunzo kwa mkulima, Epaphras Mwilambwe amesema mbegu hiyo ina muda wa miaka miwili kwa mikoa ya Tabora na Kigoma huku wakulima 2,000 wakifikiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live