Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima waaswa kukatia Bima mazao yao

Wakulima Waaswa Kukatia Bima Mazao Yao Wakulima waaswa kukatia Bima mazao yao

Thu, 18 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amewahimiza wakulima kutumia bidhaa na huduma za bima za kilimo kwaajili ya kujikinga na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko,ukame na wadudu waharibifu.

Dkt. Saqware amesema hayo jana Aprili 17, 2024 kwenye Mkutano wa elimu ya bima na kupokea maoni kutoka kwa wadau wa Kanda ya Ziwa uliofanyika katika Hoteli ya Gold Crest Jijini Mwanza.

Amesema wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara ikiwemo kuporomoka kiuchumi kutokana na kukosa bima ambayo ingewasaidia kufidia hasara mbalimbali wanazozipata pindi majanga yanapotokea.

“Faida za kutumia bima ni nyingi sana kwenye maisha ya watanzania inapunguza umasikini,inachochea uchumi,pamoja na kufanya biashara kuwa endelevu”, amesema Dkt. Saqware.

Aidha, amesema wanampango wa kutoa elimu kwa watanzania kama ilivyoelekezwa katika mpango wa kuendeleza sekta ya fedha nchini iliyoandaliwa na Wizara ya fedha ambapo tangu mwaka 2020 hadi 2030 wawe wamehakikisha asilimia 80 ya watanzania wanaelimu ya bima na asilimia 50 wanatumia bidhaa za bima kutoka kwa watoa huduma ambao wamepewa leseni na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).

Meneja wa Kanda ya Ziwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Richard Toyota amesema suala la uelewa wa bima bado liko chini kwani ni asilimia 15 ya watanzania ndio wanauelewa wa bima huku mchango wa Kanda ya ziwa kwenye Pato la bima kitaifa ukiwa ni asilimia 4.

“Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka 2022 Mikoa sita ya Kanda ya ziwa ina zaidi ya watu milioni 16 kama mchango wetu ni asilimia 4 kwenye Pato la taifa la bima bado ni kiwango kidogo ukilinganisha na idadi ya watu”, amesema Toyota Kwaupande wake Afisa Bima wa Kanda ya Ziwa shirika la bima la Taifa (NIC), Vincent Mushi amesema mazao waliyoyaweka kwenye bima kwa mwaka huu ni mahindi,maharage,mpunga,korosho,pamba na alizeti hivyo mteja anapopata hasara shirika litamfidia.

Mariam Meghji ni miongoni mwa watu waliopata elimu ya bima, ameomba elimu hiyo iendelee kutolewa zaidi hususani kwa watu wanaoishi vijijini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live