Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima waanza kusajiliwa kupewa ruzuku ya mbolea

Cfdcb46dd6f01a6d97642e28750588df Wakulima waanza kusajiliwa kupewa ruzuku ya mbolea

Wed, 27 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Utaratibu wa kusajili wakulima nchini kote kwenye mfumo maalumu wa kidijiti ili wanufaike na mpango wa utoaji ruzuku ya mbolea, unaanza leo katika vijiji vyote nchini.

Fomu za kuwasajili wakulima hao zitaanza kupatikana kwa watendaji wa vijiji katika maeneo yao. Aidha, uzinduzi rasmi wa mpango huo utafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha sherehe za Wakulima (Nanenane) ambazo kitaifa zitafanyika mkoani Mbeya.

Hayo yamebainishwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Stephan Ngailo wakati akitangaza hatua zilizochukuliwa na serikali kusaidia wakulima katika msimu wa kilimo 2022/23.

Dk Ngailo alisema kutokana na athari za janga na virusi vya corona (Covid-19) na vita kati ya Urusi na Ukraine, bei za mbolea zimeendelea kupanda ikilinganishwa na mwaka 2020.

Alisema wastani wa bei ya mbolea aina ya DAP hadi kufika nchini ilikuwa Dola za Marekani 410 kwa tani mwaka 2020, lakini mbolea iliyoingia nchini Juni mwaka huu kwa kiwango hicho ilikuwa Dola za Marekani 830 sawa na ongezeko la asilimia 168.

“Bei hii imeathiri wakulima na sasa mfuko mmoja wa mbolea hiyo aina ya DAP imepanda kutoka Sh 55,843 kwa mfuko wa kilogramu 50 Juni mwaka 2020 hadi kufikia Sh 126,607 Juni 2022,” alisema Dk Ngailo.

Alisema serikali imeliona hilo na katika bajeti ya mwaka huu wa fedha ya Wizara ya Kilimo, Sh bilioni 150 zimetengwa kugharamia ruzuku ya mbolea itakayotolewa kwa wakulima wote nchini.

Alisema lengo la ruzuku hiyo ni kupunguza makali ya bei ya mbolea, kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani.

Dk Ngailo alisema aina za mbolea zitakazohusika kwenye rukuzu hiyo ni za kupandia aina ya DAP na UREA kwa ajili ya kukuzia ambazo ni sawa na asilimia 50 ya matumizi yote ya mbolea nchini.

Alisema aina nyingine ya mbolea za kupandia na kukuzia zitahusishwa kwenye ruzuku hiyo ikiwamo ya Minjingu na ya kiwanda kipya mkoani Dodoma na zitaingizwa kulingana na mahitaji ya soko.

Alisema kutokana na uzoefu wa utoaji ruzuku miaka iliyopita, serikali imeamua kutumia mfumo wa kidijiti kuratibu shughuli zote za utekelezaji wa mpango huo na kuanzia leo wakulima wote wataanza kusajiliwa katika ofisi za watendaji wa vijiji katika maeneo yao.

“Katika kutekeleza hili, wakulima wote wanaotaka kupata ruzuku ya mbolea lazima wasajiliwe na fomu tunaanza kuzisambaza kesho (leo) katika ofisi zote za watendaji wa vijiji,” alisema Dk Ngailo.

Alisema katika mpango huo, wadau wote wa mbolea watahusishwa wakiwamo wazalishaji, waingizaji mbolea, mawakala, kampuni na wafanyabiashara ambao kila mkulima atakuwa na namba ya utambulisho itakayotumika akihitaji kununua mbolea ya ruzuku.

Kadhalika, mbolea ya ruzuku itakuwa na namba maalumu yaani QR code na itawekwa kwenye mbolea ya kilogramu 25 na ya kilogramu 50 na kuchapwa nembo ya Mbolea ya Ruzuku.

Mtendaji huyo wa TFRA hakutaja kiwango cha bei ambacho mkulima atapaswa kuongeza kwenye mfuko mmoja wa mbolea, akisema bei ya mbolea ya rukuzu itatolewa baadaye na kuwa hivi sasa wakulima waendelee kujisajili ili kuingia katika mpango huo.

Alitoa angalizo kwa wakulima na wadau wa mbolea kuwa ili kupata mbolea hiyo ni lazima wakulima wawe wamejisajili, na kuwahimiza kuanza kufanya hivyo mapema kuepuka kusubiri siku za mwishoni.

“Wakulima wasiwe na wasiwasi, tunafahamu kuwa mkulima anaweza kuwa na mashamba katika mikoa tofauti au maeneo tofauti, cha msingi ni lazima unaposajili toa taarifa na kuna eneo utajaza katika fomu hiyo kuonesha kuwa una eneo jingine mahali fulani, ili liweze kupata mbolea katika maeneo yote unayolima,” alifafanua Dk Ngailo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live