Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa zabibu nao walia

26631 Pic+zabibu TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati sakata la mauzo ya korosho likiwa limepamba moto, limeibuka jambo jingine la bei ndogo ya zabibu mkoani Dodoma.

Takribani minada mitatu ya korosho imevunjika kutokana na wanunuzi kutoa bei ndogo ambayo wakulima wameikataa na hivyo kusababisha Serikali kuingilia kati na kuwapa siku nne wafanyabiashara hao ‘kujisalimisha’ kwa Waziri Mkuu kwa kumuandikia barua wajieleze kiwango watakachonunua. Agizo hilo linamalizika leo saa 10 jioni.

Lakini, wakati Serikali ikiwa inajiandaa kununua korosho hizo kama wanunuzi hawatajitokeza, kuna mzozo mkoani Dodoma ambako wakulima hawaridhishwi na bei ya Sh1,000 kwa kilo baada ya msimu uliopita kuuza hadi Sh3,200 kwa kilo.

Zabibu ni miongoni mwa mazao yanayopewa kipaumbele na wakulima mkoani hapa ambako zabibu huvunwa mara mbili kwa mwaka tofauti na sehemu nyingine duniani.

Tangu zao hilo lilipoingizwa na wamisionari miaka ya hamsini na baadaye Serikali kuweka msukumo baada ya uhuru, zabibu imekuwa moja ya mazao makubwa mkoani Dodoma ambako sasa viwanda vitatu vikubwa vimeshajengwa kwa ajili ya kununua na kuchakata ili kupata mvinyo.

“Hakuna tunachokipata katika bei hiyo kwa kuwa hata hiyo Sh1,000 inatajwa, lakini kwa uhalisia tunauza Sh800 (kwa kilo) kwa kubembeleza ili mazao yasiozee shambani,” anasema Jackson Lusinde, mkulima wa kijiji cha Mvumi, Ilolo ambako zabibu hulimwa kwa wingi.

“Tumaini la kupata faida halipo tena na sina mpango wa kuendeleza mashamba zaidi kama nilivyokuwa nimejiandaa.

“Naona hili zao linageuka kuwa laana. Natamani kama ningepata nafasi nibebe zabibu nikagawe kwa watoto yatima au niwapelekee wabunge maboksi mengi wakagawe kwao, naumia sana.”

Lusinde alikuwa na uhakika wa kuvuna zaidi ya tani 10, lakini matarajio hayo sasa yanatoweka.

Mkulima mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Isaya Ndahani anasema hana mpango wa kulima zao lolote la biashara kwa sasa kwa kuwa anajua imekuwa ni kama danganya toto kwa wakulima kuuza walivyo navyo na kuwekeza kwenye mazao ya biashara, lakini mwisho wake unakuwa ni mbaya.

Suala hilo pia limemgusa mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliyesema hali ni mbaya kwa wakulima kwa kuwa wengi waliwekeza nguvu zao kwenye zabibu kwa kuzingatia bei ya mwaka jana wakiamini kuwa mwaka huu ingekuwa kubwa zaidi.

Lusinde alisema tegemeo la watu wa Dodoma kufikia uchumi wa viwanda ni zao la zabibu.

“Serikali imehamasisha sana watu walime, kumbe hakuna maandalizi ya kununua mazao yao,” alisema mbunge huyo.

“Lakini kuna tetesi ambazo tunazisikia kwamba kuna mchuzi (malighafi) wa zabibu unatoka nje ya nchi na hivyo kufanya soko la wakulima wetu lififie. Hilo linatuumiza na Serikali ilipaswa kutoa majibu kama wakulima waachane kabisa na zabibu.”

Kwa sasa kuna viwanda vitatu vya zabibu mkoani Dodoma ambavyo ni Dodoma Wine (Dowico), Central Tanzania Wine (Cetawico) na Alko Vintages ambavyo kwa pamoja vilisaidia uzalishaji wa zabibu kuongezeka kutoka tani 8,368 mwaka 2011/12 hadi matarajio ya tani 16,637 msimu wa 2018/19.

Hata hivyo, uwezo wa viwanda kuchakata zao hilo ni asilimia 27 tu ya mazao yanayozalishwa.

Mkurugenzi wa kiwanda cha Cetawico, Catherine Mwimbe anasema uwezekano wa kununua zabibu yote kutoka mashambani ni mdogo kutokana na hali halisi ya soko kwa sasa.

Mwimbe anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo kwenye soko ni utitiri wa kodi zinazosababisha uzalishaji kuwa ghali kulinganisha na nchi nyingine, kama Afrika Kusini.

“Siwezi kukutajia kodi zote, lakini ninukuu; nikikuambia tuna kodi nyingi kubaliana na kauli hiyo, tena sasa tunabanwa zaidi kwenye vifungashio, hasa chupa ambazo tunaagiza kutoka Afrika Kusini,” alisema Mwimbe.

Anasema ili mfanyabiashara wa Tanzania apate faida, chupa ya mvinyo ilitakiwa iuzwe Sh10,000 na hivyo ingekuwa ghali madukani. Anasema chupa ya ujazo kama huo kutoka Afrika Kusini inauzwa Sh8,500.

Mwimbe anasema kilio cha kodi walishakipeleka siku nyingi serikalini, lakini hawajaona mrejesho. Hali hiyo imesababisha washushe uzalishaji na kupunguza wafanyakazi.

Anasema mwaka 2017, Cetawico ilinunua tani 1,186 lakini mwaka huu imenunua tani 500 tu na pia mwaka 2016 waliuza lita milioni 1.3 za mvinyo, lakini mwaka huu wameuza lita 1,800.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge aliitisha kikao kilichohusisha wakulima na wenye viwanda Septemba akiwahisi wanunuzi kuwanusuru wakulima hao wa zabibu.



Chanzo: mwananchi.co.tz