Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa tumbaku wapewa Bil. 86

Tumbakuu.jpeg Wakulima wa tumbaku wapewa Bil. 86

Fri, 15 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kampuni ya kununua na usindikaji tumbaku nchini ya Alliance One Tobacco Tanzania Ltd, (AOTTL) yenye makao makuu yake mjini hapa imelipa Sh.bil 86 kwa wakulima ilioingia nao mkataba kwa msimu wa zao hilo kwa mwaka 2022.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ephraim Mapoore wakati akimpa taarifa Mkuu wa MKoa wa Morogoro, Martin Shigella ambaye alifanya ziara kiwandani hapo ili kuzindua msimu wa uchakataji zao hilo.

Alisema wamelipa fedha hizo baada ya kununua kilo milioni 22 za tumbaku kutoka kwa wakulima 11,000 ambao wanatoka katika vyama vya msingi vya wakulima zaidi ya 150.

“Tumelipa zaidi ya Sh bilioni 86 kwa wakulima hao 11,000 kutoka maeneo mbalimbali yanayolima tumbaku nchini, kama kampuni tumedhamiria kuona tunabadili maisha ya wakulima wetu na familia zao,” alisema.

Mkurugenzi huyo mtendaji pia alisema kwa kipindi cha miaka mitano imetumia Sh bil 26.5 kama mishahara na marupurupu mengine kwa wafanyakazi wake.

Kampuni hiyo inawafanyakazi wa kudumu 350 na huajiri wengine 3,000 wakati wa msimu wa tumbaku.

AOTTL ambayo ni kampuni tanzu ya Alliance One International (AOI) yenye makao makuu yake North Carolina, Marekani pia katika miaka mitano iliyopita kila mwaka imekuwa ikilipa kodi mbalimbali zinazohusiana na ajira za Sh bil 11.6 na kupeleka katika mifuko ya hifadhi ya jamii bilioni 1.718 kila mwaka.

Pia kampuni inasaidia katika kuinua pato la taifa kwa kuchangia asilimia 3 za tozo inazotakiwa kulipa katika wilaya inakonunua tumbaku, kukamilisha tozo ya hifadhi kwa vyama vya msingi ya dola 0.07 kwa kila kilo ya tumbaku iliyonunuliwa huku tozo kwa vyama vikuu vya ushirika vya WETCU, LACTU, KATCU, na CETCU zikilipwa dola za Marekani 0.023 kwa kila kilo iliyonunuliwa.

Amesema kampuni hiyo imejikita katika kusaidia jamii maeneo mbalimbali ikiwemo ufadhili wa mbio za Mwenge Mwenge wa Uhuru katika wilaya 15 ambazo ipo na kusaidia hospitali kuu ya Morogoro vifa tiba, kukabiliana na janga la Covid-19 na kukarabati na kujenga shule mbalimbali mjini humo.

Pamoja na mafanikio yote hayo kampuni hiyo imeelezea changamoto kadha zinazowakabili ikiwemo umeme usiokuwa wa uhakika wa Tanesco ingawa wanalipa Sh bil 1.4 kila mwaka.

Imeelezwa kuwa asilimia 31 ya matumizi ya umeme katika kiwanda chake unafuliwa na jenereta lake na hivyo Tanesco kukosa mapato.

Aidha kuna tatizo la maunganisho ya maji kutoka MORUWASA kwenda kiwandani na pia kuwepo na kodi nyingi ambazo zimesababisha gharama kuwa juu kwa asilimia 30.

Aidha alisema kwamba wamekuwa na mzozo na Mamlaka ya Mapato nchini kuhusu masuala mbalimbvali ya ulipaji wa kodi

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Martin Shigella alipongeza kampuni hiyo kwa juhudi kubwa inayofanya kuboresha maisha ya wakulima wa tumbaku na wafanyakazi wake tangu wamenza shughuli zao mwaka 1998.

Alisema ziara yake kiwandani hapo ni kutekeleza maagizo ya Rais Samia Sulkuhu Hassan ya kutaka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha kwamba wanatembelea wawekezaji na kutatua matatizo yao.

Alihakikishia wawekezaji hao kwamba tatizo lao la umeme na maji litatuliwa haraka.

Aidha aliahidi kuzungumza na watu wa TRA kuona ni namna gani wanaweza kufikia muafaka kuhusu masuala ya kodi kwa kuangalia pia agizo la Rais Samia alililolitoa hivi karivuuni alipokuwa katika ziara ya mkoa wa Kagera.

Alisema mkuu wa mkoa huyo kwamba ni vyema viwanda kama hicho vikasaidiwa ili kuongeza tija.

“Ni vyema tukasaidia viwanda hivi na kuhakikisha wanaongeza tija kutoka kuchakata kilo milioni 70,000 hadi zaidi ya kilo milioni 150,000” alisema Shigella.

AOTTL ilianzishwa nchini Tanzania mwaka 1988 baada ya kuungana kwa

DIMON Incorporated na Standard Commercial Corporation (STANCOM) zote za Marekani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live