Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa tumbaku Tabora wadai Sh1 bilioni

TUMBAKU 2 Wakulima wa tumbaku Tabora wadai Sh1 bilioni

Thu, 16 Feb 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wakulima wa tumbaku wilayani Uyui, mkoani Tabora, wanaidai kampuni ya ununuzi ya tumbaku ya PCL zaidi ya Sh1.02 bilioni baada ya kuiuzia tumbaku msimu 2021/22.

Akitoa taarifa ya kilimo cha tumbaku wilayani humo leo Februari 15, mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji, Brighton Kilimba, amesema wakulima wanadai kwa muda mrefu sasa hilo deni lao na hawajui hatma yao.

"Wakulima wanadai kwa muda mrefu na kwa kweli hawaelewi kama watalipwa na tunaomba Serikali isaidie wapate malipo yao," amesema.

Kwa upande wa changamoto zingine amezitaja kuwa ni baadhi ya wanachama kutokuwa waaminifu kwa kutorosha tumbaku na kusababisha kulaza madeni kwenye taasisi za kifedha na wakulima kutolipana kwa asilimia 100.

Kuhusu mikakati ya kushughulikia changamoto za zao hilo, Kilimba ameeleza kuwa wameunda kikosi kazi cha zao la tumbaku kwa ajili ya kuboresha zao hilo sanjali na kushughulikia utoroshaji wa zao hilo kwenye vyama vya msingi.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Igoko, wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian, amewaonya kuachana na tabia ya utoroshaji wa tumbaku, akisema ni tabia mbaya na lazima ikomeshwe.

"Kwa kutorosha tumbaku mnakuwa pia mnakwamisha hata mapato ya halmashauri na vyama vya msingi," amewaeleza.

Mkuu huyo wa mkoa, amewapongeza kwa kazi nzuri kwani wamelima tumbaku vizuri na matarajio ni makubwa kuvuna kwa wingi na kupata mavuno mengi na bei nzuri.

Amewaahidi kuwa watauza tumbaku yao kwani makampuni ni mengi ya ununuzi wa tumbaku na mengine yatazidi. Kuja kiasi kwamba sasa wataondokana na tumbaku yao kutonunuliwa kama zamani kwa tumbaku ile iliyozidi.

Mkuu wa mkoa yupo katika ziara ya kutembelea wakulima wa tumbaku na kuzungumza nao kufahamu changamoto zao kwa lengo la kuzitatua.

Chanzo: mwanachidigital