Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa parachichi Njombe, waanzisha Saccos kujikwamua

Tanzania Nchi Ya Tatu Kwa Kilimo Cha Parachichi Wakulima wa parachichi Njombe, waanzisha Saccos kujikwamua

Fri, 19 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ili kuondoka na tatizo la kutokopesheka kunatokana na masharti magumu, wakulima wa parachichi mkoani hapa wameanzisha Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos), kikilenga kuwasaidia wakulima wadogo wa zao hilo.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa asasi ya wakulima wa parachichi Nyanda za Juu Kusini (NSHIDA), Frank Msigwa kwenye mkutano wa wakulima wa zao hilo uliofanyika mkoani hapa.

Amesema sababu ya kuanzisha Saccos hiyo ni asilimia 95 ya wakulima wa parachichi mkoani humo hawana sifa ya kukopesheka kwenye benki. “Licha ya kufanya juhudi kadhaa ili kuhakikisha wanakopesheka ni asilimia tano tu ya wakulima wa zao hilo wamefanikiwa kupata mikopo.

"Tukiwa na Saccos hii tunamkopesha mkulima hata mwenye mti mmoja wa parachichi kwa masharti nafuu kwa kuwa ni benki yetu sisi wenyewe na tunafahamiana," amesema Msigwa.

Amesema wakulima wanastahili kukopesheka kwa sababu wana uwezo wa kulipa kutokana na ukweli kuwa soko la zao hilo ni la uhakika.

Aidha amesema kuna zaidi ya kampuni 15 mkoani Njombe zilizofika kwa ajili ya kununua parachichi, iwapo mkulima atawezeshwa kwenye miundombinu ya maji, pembejeo na dawa, atazalisha mazao bora na kuuza kirahisi.

Ofisa Ushirika wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Idd Chamshama amesema Serikali inatambua kuwa ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwezesha wananchi kiuchumi hasa wakulima wadogo.

Amesema jukumu la Serikali ni kuendelea kuhamasisha wananchi kuanzisha vyama vya ushirika kwa malengo ya kujikomboa na umasikini na kuboresha maisha yao.

"Kwa hiyo Serikali kupitia Sera ya Maendeleo ya Ushirika, inahimiza uanzishwaji wa vyama vya ushirika ambavyo ni imara na endelevu, vitakavyokidhi matarajio ya wanachama" amesema Chamshama.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Njombe Mjini, Alatanga Nyagawa amesema ili wakulima wa zao hilo mkoani humo waweze kukua kiuchumi na kutatua changamoto zinazowakabili, ni lazima waungane.

"Fursa tulizonazo kwenye parachichi ni lazima tuzitumie kwa kutafuta masoko ya uhakika ili wakulima wetu wakue kiuchumi," amesema Nyagawa.

Akizungumzia hilo, mkulima wa parachichi Tumaini Mhoka amesema kuanzishwa kwa chama hicho kutawasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuwa na masoko ya uhakika.

"Ukienda benki unaambiwa ulete dhamana, mara hati ya vitu mbalimbali jambo ambalo ni gumu kwa wakulima. Ukifanikiwa kuchukua mkopo mwezi unaofuata unaambiwa uanze kulipa wakati unategemea ulime uvune kisha ndiyo uuze na kulipa madeni," amesema Mhoka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live