Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa mikoa tisa wanufaika na miche ya viungo

Viungo Miche Wakulima wa mikoa tisa wanufaika na miche ya viungo

Mon, 15 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima wa mikoa tisa ya Tanzania Bara wamenufaika na upandaji wa miti ya matunda na viungo baada ya Kituo cha Utafiti cha Tari Mlingano kilichopo wilayani Muheza mkoani Tanga, kugawa miche bure.

Imeelezwa kuwa hizo ni jitihada za kutunza mazingira na kuimarisha lishe bora zinazofanywa na kituo hicho cha utafiti.

Mkurugenzi wa kituo cha Tari Mlingano, Catheline Senkoro ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 15, 2024 wakati akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Geofrey Mzava.

Mwenge huo umekagua vitalu vya miche ya miti, matunda na viungo kilichopo kituoni hapo.

Senkoro amesema katika kitalu hicho kuna jumla ya miche 16,153 ya kivuli viungo, mbao mpira na matunda ya aina ya milimao, miembe, michungwa, migomba na mipapai.

"Miche ya viungo ni mdalasini, karafuu, tangawizi, kokoa na kwa upande wa mbao tuna albizia, SennaSiamea, Aflezia quanzesis, tecton grands, hevea brancilesis, delonix regiu, senderea na tondoro," amesema Senkoro.

Amesema tangu kuanzishwa kwa kitalu hicho Agosti, 2021 baada ya agizo la Hussein Bashe wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Kilimo (sasa ni Waziri wa Kilimo), jumla ya miche 34,691 ya viungo na matunda imezalishwa na 13,318 imeshasambazwa kwa wakulima tangu Agosti 2021 hadi Aprili 14, 2024 katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Lindi, Mtwara, Pwani na Mbeya.

Awali, akizungumzia alipokuwa akiupokea mwenge huo, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah amesema jumla ya miradi minane yenye thamani ya Sh4.38 bilioni itafunguliwa, kuzinduliwa na kukaguliwa katika vijiji 18, vitongoji 35 na tarafa tatu za wilayani humo.

Naye Kiongozi wa mbio hizo, Mnzava amewataka wakuu wa wilaya zinazopokea Mwenge wa Uhuru kuhakikisha taarifa zinazotolewa ziendane na thamani ya fedha za miradi inayotekelezwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live