Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa matunda kupata soko Rwanda

87b7d571ea646bb80d1d4c2381a1190e Wakulima wa matunda kupata soko Rwanda

Tue, 1 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI inayosimamia wadau wa matunda, mbogamboga na viungo Tanzania (Taha) imedhamiria kukamata soko la matunda nchini Rwanda, baada ya kubaini kuwapo mahitaji makubwa ya maembe, machungwa na tufaa (apples).

Tayari taasisi hiyo imeanza mikakati ya kufuatilia soko hilo baada ya hivi karibuni kubainika nchi hiyo ina uhitaji mkubwa wa matunda hayo, ambayo yanazalishwa kwa wingi nchini.

Bodi ya Taifa ya Mazao ya Biashara Rwanda (NAEB) hivi karibuni, ilieleza kuwa licha ya kuwa na upungufu wa matunda katika soko la ndani, lakini nchi hiyo iliuza tani 8,667 za matunda kati ya Julai 2019 na Juni mwaka huu na kuingiza dola za Marekani milioni 7.5.

Mtaalamu wa Mawasiliano wa NAEB, Pie Ntwari alisema matunda mengi yanayoingizwa nchini humo, yanazalishwa bila kufuata taratibu za ubora, hivyo kushindwa kukamata soko la kimataifa. Kutokana na hali hiyo wanasambaza mbegu bora ili wakulima wazalishe matunda bora.

Taha imesema baada ya kuona taarifa hizo, itawasiliana na taasisi husika za biashara nchini Rwanda, kubaini aina ya matunda yanayohitajika, bei na kiwango kinachohitajika ili kuwawezesha wakulima wa Tanzania kukamata fursa hiyo.

Meneja Uzalishaji na Masoko wa Taha, Emmanuel Faustine alisema katika miaka ya karibuni, wamekuwa wakiuza mazao mbalimbali nchini Rwanda, ikiwamo mahindi na soya, lakini hawajawahi kufanya biashara za matunda nchini humo.

Alitaja nchi wanazouza bidhaa kwa wingi kama vitunguu, maua, maharage, matunda na mboga, viazi na mengineyo kuwa ni Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Comoro.

Chanzo: habarileo.co.tz