Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa korosho wapewa darasa la biashara

Mwenyeji Korosho Wakulima wa korosho wapewa darasa la biashara

Wed, 13 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati msimu wa korosho ukielekea ukingoni, wakulima wa zao hilo wametakiwa kutumia vizuri fedha walizopata kwa kununua chakula, kuboresha makazi na mahitaji mengine muhimu ikiwemo sare za wanafunzi na siyo kucheza unyago.

Rai hiyo imetolewa leo, Jumanne Desemba 12, 2023, katika mnada wa nane, uliofanyika katika Kijiji cha Chenjele na Kaimu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Runali, Shamsia Namtonga ambaye amewataka wakulima waweke akiba ya fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu.

“Msimu wa korosho ndiyo unaelekea ukingoni, ni vema mkaweka akiba ya fedha kwaajili ya kununua chakula na mahitaji muhimu ya familia, msisahau sare za shule kwa watoto na kuboresha makazi,” amesema Shamsia.

Shamsia amesema wengi wa wakulima hutumia fedha zao kwa kucheza unyago huku wakisahau mahitaji muhimu ya familia, hivyo, asingependa kuona jambo hilo linatokea kwa wakulima ambao ni wanachama wa chama hicho kinachojumuisha Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale.

"Pia niwaombe wakulima wenzangu, hivi sasa tunakwenda kwenye minada ya mwishoni na kwakuwa tuko katika msimu wa mvua, basi tujitahidi kupeleka korosho zetu kwenye maghala,” amesema Shamsia.

Kwa upande wa Ofisa Ushirika Mkoa wa Lindi, Projestus Pascal amesema kuwa viongozi wa vyama vya msingi (Amcos), wajitahidi kuwalipa wakulima fedha zao kwa wakati na huku akisisitiza kwa wakulima walio na korosho majumbani wazihifadhi katika maghala, wakisubiri minada ya mwisho.

"Ni vema pia korosho zilizoko nyumbani, tuhakikishe zina anikwa vizuri ili kuepuka kupeleka korosho yenye unyevu," amesema Projestus.

Naye Mhasibu Mkuu wa Runali, Hashimu Abdalla amesema kuwa kampuni 13 ziliomba kununua korosho tani 100,000 na kwamba zimeuzwa kwa bei ya juu ya chini kwa Sh1,840 na Sh1, 660 mtawalia.

Mkulima wa zao la korosho kutoka kijiji cha Chienjele, Elias Swedy amelalamikia bei akisema haikuwa nzuri na hivyo kuitaka Serikali kujitahidi kuongeza bei kwenye zao hilo kutokana na na mchakato wake katika uzalishaji kuwa mgumu.

"Kwanza niishukuru Serikali, kiukweli malipo ya sisi wakulima yanakwenda vizuri ila niiombe Serikali kwenye swala zima la bei, sio nzuri sana, mchakato wa zao la korosho ni mgumu, tunakubali kuuza kwa bei isiyoridhisha kwa sababu tukiziacha hatuna pakuzipeleka," amesema Elias.

Mkulima Mwajuma Libaba, ameiomba Serikali kuongea na wanunuzi huku akiamini ushindani unaweza kuleta matumaini kwao kwa bei kuwa nzuri.

“Ulimaji wa korosho ni mgumu sana, ukianzia pembejeo, kupulizia hadi kuja kwenye kuvuna, hizi bei zinazopatika kwenye minada, hazituridhishi ila hatuna namna tunakubali kuuza, tukikataa tutamuuzia nani?" amehoji Mwajuma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live