Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa korosho wakataa kupunjwa bei

6b2ab911f04d784eee5911f5689a30c2 Wakulima wa korosho wakataa kupunjwa bei

Sat, 24 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKULIMA wa korosho mkoani Ruvuma wamegoma kuuza korosho zao katika mnada wa kwanza katika msimu wa 2020 uliofanyika katika Kijiji cha Muhesi baada ya wanunuzi kutangaza kununua zao hilo kwa bei ndogo isiyolingana na gharama ya uzalishaji.

Katika mnada huo, kampuni mbili zilijitokeza kununua korosho kwa bei kati ya Sh 2,180 hadi Sh 2,350 bei ambayo ni ndogo ikilinganishwa na bei ya korosho ya Sh 2,700 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Wakizungumza jana mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Julius Mtatiro, wakulima hao walisema bei iliyotangazwa na wanunuzi ni ndogo, hivyo hawako tayari kuuza hadi pale itakapotangazwa bei nzuri katika mnada wa pili utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru (TAMCU) Ltd, Hashim Mbalabala, alisema haiwezekani wakulima kuuza korosho kwa bei ya kutupa na kuwataka wanunuzi kuangalia upya bei hiyo kwani wakulima wamekuwa wakifanya shughuli zao za kilimo katika mazingira magumu na kwa gharama kubwa.

Alisema bei ya wanunuzi hao haina faida kwa wakulima, hivyo hakuna mkulima aliyekubali kuuza korosho kwa bei ndogo na kuwataka wanunuzi hao kujitafakari kama kweli wana lengo la kununua.

Mkulima ambaye ni mwanachama wa Namiungo Amcos, Juma Bakari, alisema bei iliyotolewa na wanunuzi imewavunja moyo kwani hailingani na gharama za kuandaa mashamba hadi kufikia hatua ya kuuza.

Alisema kuliko kuuza korosho kwa bei ya chini, bora wabaki nazo majumbani kwa kuwa hawataweza kulipia pembejeo walizokopa kwa wafanyabiashara.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa TAMCU wilayani Tunduru, Imani Kalembo alisema hadi kufikia juzi zaidi ya tani 1,902 ziliingizwa katika mnada wa kwanza wa korosho msimu 2020.

Kwa mujibu wa Kalembo, licha ya changamoto zilizojitokeza, wanategemea kupata korosho nyingi kutoka katika vyama vya msingi vya ushirika ambapo wakulima wanaendelea kupeleka korosho zao kwa ajili ya kuuza katika minada inayofuata.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, ameagiza minada inayofuata wanunuzi kuweka bei nzuri ambayo itawanufaisha wakulima kama ilivyo katika minada iliyofanyika katika mikoa jirani ya Lindi na Mtwara ambapo bei ya korosho ilikuwa kati ya Sh 2,500 hadi Sh 2,700.

Alisema kama wanunuzi hawatakubali kuweka bei nzuri, Serikali ya Wilaya inaweza kuweka utaratibu mwingine wa kuuza korosho ambao utawasaidia wakulima wa wilaya hiyo badala ya kuendelea na wafanya biashara ambao wana lengo la kurudisha nyuma juhudi za wakulima.

“Kimsingi bei zilizoletwa na wanunuzi katika mnada wetu wa leo siyo rafiki kabisa kwa mkulima na hazileti mahusiano mazuri kati yao na wakulima, hizi siyo bei sahihi hata kidogo ni lazima wanunuzi wajitafakari kama kweli wana nia ya kununua korosho zinazolimwa katika Wilaya yetu,” alisema.

Pia amepiga marufuku wafanyabiashara kwenda kununua korosho katika vyama vya msingi vya ushirika, badala yake kuelekeza wafanyabiashara wote kununua korosho ambazo zimeingizwa katika maghala maalumu yaliyoteuliwa.

Chanzo: habarileo.co.tz