Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa choroko wagoma kuuza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani

Koroshoo Wakulima wa choroko wagoma kuuza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani

Sat, 6 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Wakulima wa choroko mkoani Singida wamegoma kuuza zao hilo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani baada ya mnunuzi aliyejitokeza kutofikia bei waliyoitaka.

Hayo yamejiri leo Aprili 5, 2024 katika ghala la kuhifadhia mazao la Nselembe lililopo Shelui wilayani Iramba, mkoani Singida baada ya kufanyika mnada kwa njia ya mtandao.

Alijitokeza mnunuzi mmoja aliyetaka kununua kwa Sh1, 010, bei ambayo wakulima hawakuiridhia wakisema haina masilahi kwao.

Choroko hizo takribani tani 50 zilikusanywa na wakulima kwa kushirikiana na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Singida na Halmashauri ya Iramba kwa lengo la kuziuza kwa njia ya stakabadhi ghalani.

Elibariki Issa, mkulima aliyehudhuria mnada huo amesema bei iliyofikiwa ni ndogo, hivyo kutaka mnada urudiwe.

Mariam Haji amesema choroko zake zimekaa takribani wiki tatu sasa katika ghala hilo wakisubiri mnada ambao bei iliyotolewa ni ndogo.

Emmanuel Benjamin, amesema mfumo huo unawakandamiza kutokana na wakulima kulazimishwa kukusanya na kuuza.

“Huu mfumo ni kandamizi na hautendi haki, nashauri waruhusu AMCOS ziendelee na wafanyabiashara, mkulima ataona wapi kuna faida,” amesema.

Wakulima wamekubaliana mnada urudiwe Jumatatu Aprili 8, 2024.

Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Iramba, Marietha Kasongo amesema licha ya wakulima kutoridhishwa na mfumo huo, maagizo aliyopewa na mkuu wa wilaya hiyo ni kwamba, hata yeye hajaridhishwa na bei iliyofikiwa lakini bado mfumo huo utaendelea kutumika.

“Mnada utarudiwa na utafanyika haraka, tamko alilolisema mkuu wa wilaya ni kwamba hata yeye hajaridhika na bei hiyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Singida, Yahaya Ramadhani amesema kilichofanyika ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuuza kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na baada ya wakulima kutoikubali bei, utaratibu unataka mzigo utangazwe upya ili uuzwe tena na bei ikiridhiwa na wakulima mzigo utauzwa au waruhusu njia nyingine ya mnunuzi kutuma barua yenye bei kama njia mbadala.

Kuhusu kujitokeza mnunuzi mmoja, jambo lililolalamikiwa amesema wao kama chama hawana mamlaka ya kutangaza mzigo wala kutafuta wanunuzi, wenye mamlaka hayo ya kutangaza ni Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

“Ni agizo la kimkoa Serikali ilishaamua hivyo, sisi tumekuja kutekeleza, bei imefika ni ndogo, wakulima wameikataa, sasa baada ya kushindikana utaratibu ni kuwaomba tena TMX wauweke tena mzigo sokoni ili uuzwe kama utafika bei nzuri utauzwa sasa kuna njia nyingine ambayo inaitwa ‘Inbox’ ambayo mnunuzi anatuma barua anataja mwenyewe bei yake ambayo inakuwa ni siri yake, akijumuisha na bei ambayo imepangwa na Serikali,” amesema.

Chanzo: Mwananchi