Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima mvua hizi zisipite hivihivi

4ebf2dc6c515481911c9d23724e675f4.jpeg Wakulima mvua hizi zisipite hivihivi

Wed, 15 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kipindi kirefu cha kukosekana mvua, hatimaye maeneo mbalimbali nchini kwa sasa yamekuwa yakipata mvua jambo ambalo ni neema hasa kwa wakulima na sekta nyingine zinazotegemea maji.

Kukosekana kwa mvua kwa kipindi kirefu kilichopita kumesababisha changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa maji, kusuasua kwa uzalishaji umeme, uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo na madhila mengineyo. Hali hiyo ya ukosefu wa mvua ilianza kuwatia wasiwasi wakulima na wadau wengine na hata serikali kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi na kusababisha uhaba wa chakula na huduma nyingine za kijamii kama maji na nishati ya umeme kuzidi kudorora.

Kwa mujibu ya utabiri wa hali ya hewa uliotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua hizi zitaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ni neema ambayo haipaswi kuachwa ipotee hivihivi hasa kwa wakulima kwa kuzingatia ukosefu wa mvua huko nyuma.

Hii ni neema ambayo inapaswa kutumiwa vizuri na jamii, serikali na hasa wakulima kuhakikisha wanapanda mazao mbalimbali kwa wingi ili kupata mavuno mengi. Rai yetu ni kwamba, wakulima watumie mvua hizi kupanda mazao mbalimbali hasa yanayokomaa haraka ili kupata mavuno mengi ili kuondoa adha ya uhaba wa chakula, pamoja na kupata ziada ya kuuza na kujipatia kipato.

Kwa upande mwingine, tunawasihi wataalamu wa kilimo hasa maofisa ugani huu si muda wa kukaa ofisini, bali wanatakiwa kwenda kwa wakulima kuwasaidia na kuwapa ushauri juu ya ni mazao gani yanapaswa kupandwa kwa kutumia mvua hizi. Pia wataalamu hao wanatakiwa kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya pembejeo mbalimbali za kilimo hasa matumizi ya mbolea ili waweze kuendesha kilimo cha kisasa na chenye tija.

Aidha, kutokana na hali ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha mvua kuwa haba, wataalamu wa kilimo wanatakiwa kuwashauri na kuwaelekeza wakulima na serikali kwa ujumla jinsi ya kuhifadhi maji ya mvua zinaponyesha ikiwamo uchimbaji wa mabwawa ili maji yatakayopatikana yaweze kuja kutumika kumwagilia mazao wakati wa kiangazi.

Hali hiyo itawahakikishia wakulima kuwa na chakula cha kutosha wakati wote na kuondoa hofu ya uhaba wa chakula inayojitokeza mara kwa mara mvua zinapokosekana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live