Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima kuuza mazao kwa njia ya posta

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirika la Posta linatarajia kutoa huduma ya kuuza bidhaa mbalimbali kwenye mtandao ikiwamo mazao kwa njia ya posta.

Hayo yamesemwa leo Julai 10 na Kaimu Meneja Rasilimali wa  Shirika hilo, Morice Mbodo alipokuwa akiwasilisha taarifa za shirika hilo na mikakati yao ya baadaye mbele ya kamati ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea shirika hilo.

Mbodo amesema hatua hiyo ni baada ya shirika kujiunga katika mtandao wa huduma za posta na nchi nyingine 150 duniani ambapo watakuwa wakifanya biashara ya kimtandao kwa kuuza bidhaa mbalimbali.

"Biashara hii ya kimtandao ni kweli inafanywa na watu wengi, lakini sisi tumeenda mbali zaidi hadi kuwafikia wakulima na wajasiriamali wadogo kuuza bidhaa zao ukizingatia tuna mtandao mpana sio tu nchini bali na duniani.

 

 

“Tunaomba wakulima na wafanyabiashara wa mazao tutakapoanza kutoa huduma hii, waichangamkie ili kujikwamua na umasikini na kuinua pato la taifa kwa ujumla,"amesema Meneja huyo.

Bidhaa hizo zitasafirishwa kama kifurushi kutoka sehemu moja kwenda nyingine na mazao yatakayosafirishwa ni pamoja na nafaka na mbogamboga.

Pamoja na mafanikio hayo, amesema zipo changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwamo deni wanalowalipa wastaafu waliokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki lililofikia Sh4.9 bilioni.

Pia kucheleweshwa kwa marekebisho ya kulisimamia shirika hilo, kumelifanya kushindwa kutumia baadhi ya rasilimali kwa ajili ya kuongeza mapato.

Chanzo: mwananchi.co.tz