Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima kupewa teknolojia ya kisasa

WAKULIMA Wakulima kupewa teknolojia ya kisasa

Mon, 27 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MTAFITI wa Idara ya Uhifadhi wa Mazao na Usindikaji, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania Tari, Kituo cha Uyole kilichopo mkoani Mbeya, Dk. Andrew Urio, amewaahidi wakulima kusambaza teknolojia sahihi za uvunaji mazao ili kupunguza upotevu wa mazao wakati wa kuvuna.

Dk. Urio aliyasema hayo juzi, alipokuwa akizungumza na Nipashe juu ya mikakati waliyoiweka Tari katika kuwakwamua wakulima na tatizo la upotevu wa mazao shambani.

Alisema walianza kusambaza teknolojia ya uvunaji wa mazao shambani kwa baadhi ya wakulima pamoja na kutoa elimu ya usindikaji kwa lengo la kutunza kinachopatikana.

“Katika kutekeleza mkakati wa taifa wa kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna, tunawahamasisha wakulima kutumia teknolojia zetu sambamba na hilo pia tuliwahamasisha wajikite zaidi kwenye usindikaji wa mazao mbalimbali ili kuyaongezea thamani na kujiongezea kipato,” alisema Dk. Urio.

Aliongeza kuwa, Idara ya uhifadhi wa mazao na usindikaji ilitoa elimu ya usindikaji kwa baadhi ya mazao kama vile, soya, maharage na viazi lishe ili kutengeneza bidhaa mbalimbali, mikate, keki, bagia, maandazi, juisi na biskuti.

Alieleza umuhimu wa elimu wa kuhifadhi mazao kuwa itamuongezea mkulima uhakika wa chakula katika kaya na kuongeza thamani ya soko la bidhaa.

Hata hivyo, Dk. Urio alisema kuwa wanaendelea na mapambano dhidi ya lishe duni kwa kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi namna bora ya kuandaa chakula kitakachokuwa na virutubisho vyote muhimu ili kujenga afya.

Baadhi ya wakulima kutoka Kata ya Tembela iliyopo wilayani Mbeya, waliomba Tari- Uyole kusambaza teknolojia za uvunaji mazao kwa wakulima wote pamoja na kupunguza gharama za uuzaji.

Miongoni mwa wakulima hao, Absolom Mwandafwa, alidai teknolojia hizo huenda zikawa mkombozi kwa wakulima katika kukabiliana na tatizo la upotevu wa mazao shambani, lakini shida iliyopo hazipatikani kwa urahisi na ni ghali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live