Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima kulipwa Sh12 bilioni za korosho kila siku

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ruangwa. Ili kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho, Serikali imesema itaanza kulipa Sh12 bilioni kwa siku kuanzia wiki ijayo.

Aidha, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itajenga ghala la kisasa litagharimu Sh6.6 bilioni wilayani hapa. Alisema litakalokuwa kubwa zaidi nchini likiendeshwa kwa mfumo wa kielektroniki.

Akizungumzia malipo alisema, “Tumeshalipa Sh200 bilioni na kuanzia wiki ijayo tutaanza kulipa Sh12 bilioni kwa siku. Tawi hili pekee litakuwa linalipa kati ya Sh200 milioni na Sh300 milioni kila siku. Tunakamilisha uhakiki wa wakulima waliowasilisha zaidi ya magunia 15 ya kilo 100 kila moja,” alisema Majaliwa jana na alipokuwa akizindua tawi la Benki ya CRDB Ruangwa.

Ili kulipwa, mkulima mwenye zaidi ya tani 1.5 au magunia 15, anatakiwa kuonyesha shamba lake ikiwa ni mkakati wa kuzuia biashara ya kangomba.

Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kuwalinda wakulima ili kuongeza tija ya kilimo nchini.

Fedha kwa ajili ya kununua korosho zote zaidi ya tani 275,000 zinazotarajiwa kuvunwa ni mkopo uliotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na CRDB kwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko.

Ruangwa iliyoundwa baada ya kutenganishwa na Wilaya ya Lindi miaka 16 iliyopita, ndiyo inayoongoza kwa kilimo cha korosho na ufuta mkoani Lindi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo inahudumia vyama 12 vya ushirika vyenye jumla ya wanachama 4,600 wilayani hapa ambao wameshanufaika na mikopo ya Sh1.2 bilioni.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kufunguiliwa kwa tawi hili, tumepokea amana za Sh1.5 bilioni na kufungua akaunti 8,700. Mpaka Novemba (mwaka jana), benki ilikuwa imekopesha zaidi ya Sh16 bilioni kwa wakulima 2,900 wa Kanda ya Kusini ambao ni wanachama wa vyama vya ushirika Tandahimba na Newala (Tanecu), kwa ajili ya ununuzi wa magunia,” alisema Nsekela.

Mkurugenzi huyo alisema CRDB inaamini kwamba ili viwanda vishamiri ni muhimu kuongeza tija katika uzalishaji, usafirishaji na upatikanaji wa masoko.

“Jukumu letu ni kuhakikisha wakulima na wawekezaji wanapata mtaji wa kufanikisha malengo yao. Tumejipanga kusaidia kukuza mnyororo wa uzalishaji kuanzia kwa mkulima na kushirikiana na Serikali kuhakikisha ujenzi wa maghala ya kisasa unafanikiwa ili kuongeza tija kwa wakulima. Nafahamu maghala haya yatajengwa Ruangwa pia,” alisema Nsekela.

Licha ya mikopo ya pembejeo, CRDB imesema ipo tayari kuwawezesha wakulima kununua matrekta na magunia pamoja na ujenzi maghala kwa vyama vya msingi, vikundi na wakulima binafsi



Chanzo: mwananchi.co.tz