Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima Tunduru wavuna mbaazi za Bil. 10

Wakulima Tunduru Wavuna Mbaazi Za Bil. 10 Wakulima Tunduru wavuna mbaazi za Bil. 10

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima wa mbaazi wilayani Tunduru, wamefanikiwa kuzalisha zaidi ya kilo milioni 5,028,861 sawa na tani 5,026 zenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 10 katika msimu wa kilimo 2023/2024.

Mbaazi hizo zimeuzwa katika minada mitano kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) vikisimamiwa na Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu Ltd).

Meneja wa Tamcu Iman Kalembo alisema,wastani wa bei ya mbaazi ilikuwa Sh.1,998 kwa kilo moja ambayo ni mafanikio makubwa kwa wakulima ikilinganisha na bei ya msimu wa mwaka jana ambapo wastani wa bei ilikuwa Sh.868.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake,kwa kusimamia vema soko la zao hilo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani uliowawezesha wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri iliyowafanya wafurahie shughuli zao za kilimo.

“Rais wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutafuta soko na kuweka mfumo mzuri uliosaidia bei ya mbaazi kuongezeka kutoka Sh.868 msimu 2022/2023 hadi kufikia Sh.1,998 msimu 2023/2024”alisema Kalembo.

Kwa mujibu wa Kalembo,hapo nyuma bei ya mbaazi ilikuwa ndogo hivyo kusababisha wakulima wengi kukata tamaa ambapo amempongeza Waziri wa kilimo na Ushirika Hussen Bashe kwa kuhamasisha shughuli za kilimo hapa nchini.

Aidha,amemshukuru Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusimamia mfumo ununuzi wa mazao kupitia vyama vya ushirika na kuwaomba viongozi wa Amcos kuunga mkono jitihada hizo zinazolenga kuwasaidia wakulima.

Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule alisema,zao la mbaazi limekuwa msaada na mkombozi mkubwa kiuchumi kwa wakulima wanaosimamiwa na Chama hicho tangu ulipoanza mfumo wa stakabadhi ghalani miaka mitatu iliyopita.

Amewataka wakulima kuendelea kuvitumia vyama vyao vya ushirika na kukataa kuuza mazao nje ya mfumo wa ushirika ili kuepuka kupata hasara kutokana na kuuza kwa bei ndogo isiyolingana na gharama za uzalishaji.

Manjaule,amewahimiza wakulima wilayani humo,kulima mazao mengine ya chakula na biashara ili kujiongezea kipato kutokana na serikali kuweka mfumo mzuri uliowezesha kuwepo kwa masoko ya uhakika.

Kwa upande wake Meneja masoko wa Tamcu Marcelino Mrope alisema,tangu walipoanza kuuza mbaazi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani bei imezidi kuimarika na wakulima wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kujenga nyumba za kisasa na kuondokana na nyumba zilizojengwa kwa miti na kuezekwa na nyasi.

Amewaomba wakulima wa mbaazi kuongeza uzalishaji, ili waweze kunufaika na fursa ya uwepo wa soko la uhakika kwani Chama kikuu kina matumaini makubwa ya kuongezeka kwa bei ya zao hilo katika msimu wa 2024/2025.

Mwenyekiti wa kikundi cha wachukuzi katika ghala la chama kikuu cha ushirika Hashimu Malembe alisema,kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa katika msimu 2023/2024 wachukuzi wamenufaika kwa kupata fedha nyingi zilizowasaidia kumaliza baadhi ya changamoto kwenye familia zao.

Hata hivyo,ameiomba serikali kuendelea kuimarisha soko la zao hilo na mazao mengine yaliyoingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuwahamasisha wakulima waongeze uzalishaji kwa msimu ujao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live