Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima Tunduru watakiwa kutotegemea korosho pekee

KOROSHO 2 Wakulima Tunduru watakiwa kutotegemea korosho pekee

Thu, 6 Jan 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Wakulima wilayani Tunduru wameshauriwa kuanza kulima mazao mengine ya biashara yanayohimili ukame na kustawi vizuri ili kujiingizia kipato badala ya kutegemea zao moja la korosho.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (TAMCU Ltd), Mussa Manjaule, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa iliyosababisha mvua za masika kuchelewa kunyesha mkoani Ruvuma. Alikuwa akizungumza na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos) vinavyokusanya na kuuza korosho katika Mkoa wa Ruvuma.

Manjaule ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Korosho Tanzania alisema zao la korosho ni zao linalohitaji maji mengi hivyo kutokana na kuchelewa kwa mvua za masika ni vyema wakulima wakaanza kulima mazao mbadala yasiyohitaji maji mengi na yanayokomaa mapema.

Manjaule aliyataja mazao hayo ni pamoja na mbaazi, ufuta, karanga, alizeti na soya ambayo kama wakulima wataanza kulima katika msimu wa kilimo wa mwaka huu, kuna uhakika wa kupata fedha nyingi kutokana na kuwa na soko na kupanda kwa bei ya mazao hayo.

Aliwakumbusha wakulima kufanya palizi ya mashamba ya korosho ili mvua zitakapoanza kunyesha maji yasipotee na kuathiri shughuli za uzalishaji wa zao hilo linaloongoza kuwapatia fedha nyingi. Aidha, aliwataka viongozi wa AMCOS kuhakikisha wanalipa madeni ya pembejeo wanayodaiwa na baadhi ya kampuni.

Meneja wa Tamcu, Imani Kalembo aliwaomba viongozi wa Amcos kusimamia suala la kupeleka korosho kwenye ghala la chama hicho ili kuongeza mapato kwa chama hicho badala ya kupeleka kwenye maghala ya watu na kampuni binafsi.

Alisema inasikitisha kuona hadi sasa korosho zilizofikishwa katika ghala la Tamcu ni chache ikilinganishwa na zilizopelekwa kwenye maghala ya watu binafsi. Alisisitiza kuwa tabia hiyo inaweza kuathiri chama cha ushirika kimapato na hivyo kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake.

“Hatukatazi Amcos kupeleka korosho kwenye maghala mengine, isipokuwa ni vyema kutumia ghala la chama kikuu ambacho kinasimamia vyama vya msingi ili kusaidia kuongeza mapato ya chama,” alisema Kalembo.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alisema katika kipindi cha mwaka 2021, wilaya hiyo imefanya vizuri katika sekta ya ushirika ikiwemo kupungua kwa idadi ya Amcos zinazodaiwa fedha na wakulima kutoka 25 kati ya 35 hadi kufikia nne.

Alisema ataendelea kusimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya ushirika ili ipate mafanikio na wakulima walime kwa tija kwa kupata pembejeo kwa wakati na soko la uhakika.

Chanzo: www.habarileo.co.tz