Dar es Salaam. Wakulima nchini Tanzania wametakiwa kutumia vizuri chakula kilichopo ili kuondoa upungufu unaoweza kujitokeza hasa katika maeneo ambayo hayakupata mvua za kutosha.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Agosti 29, 2019 na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wafanyabiashara na wasindikaji wa mazao ya nafaka unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema yapo maeneo yaliyopata mazao mengi hivyo wakati wanauza mazao wakumbuke kujiwekea akiba ya chakula.
“Hatutazuia kuuza mazao ya ziada, tunafungua milango soko lipo hata kwa nchi jirani muhimu mkumbuke kuweka akiba, inawezekana sasa hivi kikaonekana kingi mkauza chote matokeo yake mkakosa kwa ajili ya matumizi ya ndani,” amesema Hasunga.
Waziri Hasunga pia ameitaja changamoto kubwa kwenye biashara ya kilimo kuwa ni kukosekana kwa takwimu zinazoonyesha kiasi na mahali yanapoweza kupatikana mahindi na mchele.
“Kukosekana kwa takwimu kunasababisha masoko kutokuwa ya uhakika. Mfano, Serikali inaweza kupata soko la mahindi nje ya nchi lakini takwimu za kufahamu ziada ilipo na hali yake inakuwa ngumu kwa sababu takwimu za wafanyabiashara binafsi hatuna.”
Pia Soma
- Ethiopia wagundua fuvu la binadamu lenye miaka milioni 3.8
- Polisi Dar yasema waliokamatwa wakiandamana kushinikiza ndege ya ATCL kuachiwa watachukuliwa hatua
- Lugola asema Tanzania ni nchi salama kwa wananchi na mali zao