Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima Mtwara waanza kwa kuuza korosho ‘kiduchu’ mnadani

25260 Korosho+pic TanzaniaWeb

Sun, 4 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zaidi ya tani 13,500 za korosho zimekosa wanunuzi katika minada iliyofanyika jana mkoani Mtwara.

Hata hivyo, wafanyabiashara wametii agizo la Serikali iliyoelekeza korosho hizo zinunuliwe kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo moja.

Licha ya mnada huo kuhudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba, kati ya tani 16,000 zilizotakiwa kuuzwa katika minada miwili iliyofanyika ni tani 2,341 (sawa na asilimia 14.6) zilizouzika.

Awali, kati ya Oktoba 20 na 24, minada mitatu ilishindwa kufanyika kutokana na wakulima kugomea bei iliyotangazwa na wanunuzi.

Meneja wa Chama cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu), Mohamed Nasoro alisema jana kuwa walipangwa kuuza tani 7,000, lakini ni 2,141 zilizouzika huku bei ya juu ikiwa Sh3,016 na ya chini Sh3,000.

Alizitaja kampuni zilizonunua kuwa ni Yaling Cashewnut iliyonunua tani 500 na Export Trading kwa Sh3,016, ilhali Kampuni ya MGM ilinunua tani 50, Royal Nuts tani 104 na Afrisan tani 317 ambazo zilinunua kwa Sh3,000. Zingine ni RCn iliyonunua tani 120, Macronmix (250) na Alfa (400) zilizonunua kwa Sh3,001, huku Kampuni ya Iscon Commodities ikinunua tani 50 kwa Sh3,005.

Meneja wa Chama cha Ushirika cha Masasi na Mtwara (Mamcu), Joseph Mnole alisema kati ya tani 9,000 zilizotarajiwa kuuzwa, tani 200 ndizo zilizonunuliwa na Kampuni ya Korosho Africa kwa bei ya Sh3,001 kwa kilo.

Oktoba 28, baada ya wakulima kugoma kuuza korosho zao wakilalamikia bei kuwa ndogo, Rais John Magufuli alifanya mkutano na wadau wa korosho katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka wafanyabiashara kununua kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo.

Katika mkutano huo uliohudhuria na wafanyabiashara, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Dk Tizeba, Rais Magufuli aliungana na wakulima kupinga bei ya wafanyabiashara ya kati ya Sh1,700 hadi Sh2,700 kwa kilo huku akisema endapo wanunuzi hawako tayari kununua Serikali itazinunua kwa bei nzui.

Chanzo: mwananchi.co.tz