Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima Mbeya kunufaika mbolea ya ruzuku

Mbolea 1 Wakulima Mbeya kunufaika mbolea ya ruzuku

Thu, 19 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aseme zaidi ya Sh200 bilioni zitatumika kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo, tayari Mkoa wa Mbeya umeneemeka na kauli hiyo kwa kupata tani 87,000 ya mbolea.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera leo Alhamisi Oktoba 19, 2023 alipofanya kikao kilichohusisha wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya, maofisa kilimo na wataalamu wa idara mbalimbali za Serikali kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya.

Homera amesema katika msimu wa kilimo 2022/23 zaidi ya wakulima 280,730 wamesajiliwa na kupata mbolea za ruzuku huku mkoa ukiwa unaongoza kwa kupata takwimu kubwa za uandikishaji.

“Mbeya tumeweza kufanya vizuri katika uandikishaji mwamko umekuwa mkubwa licha ya kuwepo kwa changamoto katika msimu wa mwaka jana katika suala zima la upatikanaji wa mbolea na kupelekea matumuzi ya mbolea kushuka kwa asilimia 70 badala ya 100,”amesema.

Amesema katika awamu hii kama Serikali wameweka vigezo kwa mawakala watakaokuwa na sifa ya kusambaza mbolea katika halmashauri zote kuhakikisha wanakuwa na vituo kwenye kila Kata ili kuwasaidia wakulima kutotumia muda mwingi kutafuta mbolea sambamba na kutembea umbali mrefu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropiki (TFRI), Anthony Diallo amesema kwa msimu wa mwaka jana chakula kiliuzwa licha ya kuwapo kwa changamoto na kuzitaka kamati za pembejeo zihusishe mawakala ili kuwafikia wakulima waweze kupata pembejeo za kilimo kwa wakati.

“Hilo litasaidia wakulima kutosafiri umbali mrefu kufuata pembejeo lengo ni kuona uzalishaji unaongezeka na kuwa na tija kubwa kwa wakulima hususan waishio vijijini,”amesema.

Naye Mwenyekiti Halmashauri ya Chunya, Bosco Mwanginde amesema kuwa mfumo wa mawakala kuweka vituo kwenye ngazi za Kata utasaidia wakulima kuondokana na usumbufu na kuishauri Serikali kutupia jicho kwenye maeneo ya vijiji vya pembezoni.

Mkulima Witness Kamwela amesema utaratibu wa Serikali ni mzuri lakini changamoto iko katika utekelezaji kwa mawakala wanaosimamia kusambaza pembejeo za ruzuku na kuomba Mkuu wa Mkoa kuweka wafuatiliaji ili kusaidia kuondoa ukiritimba kwa wasio nacho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live