Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima Mara kupewa miche milioni 1.5 ya mkonge

Miche Pic Data Wakulima Mara kupewa miche milioni 1.5 ya mkonge

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Bodi ya mkonge nchini inatarajia kugawa miche zaidi ya milioni 1.5 za mikonge katika wilaya tatu za mkoa wa Mara ikiwa ni sehemu ya maboresho ya uzalishaji wa zao hilo nchini.

Miche hiyo inatarajiwa kugawiwa bure kwa wakulima wadogo kati ya mwezi huu hadi ujao baada ya utafiti uliofanyika na kubaini kuwa zao hilo linaweza kustawi vizuri katika wilaya hizo ambazo ni pamoja na wilaya ya Rorya, Butiama na Bunda.

Akizungumza wakati wa kugawa miche katika wilaya ya Butiama, Mkuu wa udhibiti ubora Bodi ya Mkonge, Olivo Mtung'e amesema kuwa usambazaji huo unalenga kuboresha uzalishaji wa zao la mkonge na nchini kwa ujumla.

"Tuna malengo ya kuzalisha tani 120,000 ifikapo mwaka 2025 kama nchi kutoka tani 40,000 za sasa ambapo mkoa wa Mara umepewa lengo la kuzalisha tani 20,000 mwaka 2025 kutoka tani 4,000 za sasa na hii inawezekana kabisa" amesema

Amesema kuwa ili kufanikisha lengo hilo la uzalishaji wa tani 120,000 bodi ya mkonge inatarajia kutumia zaidi ya Sh212 milioni kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwaajili ya kusambaza miche ya mkonge katika wilaya 16 nchini za awamu ya kwanza kazi ambayo tayari imeanza.

Mratibu wa zao la mkonge Wilaya ya Butiama, Anatori Mfunzi ameishukuru bodi ya mkonge kwa kutoa zaidi ya miche 230,000 kwa wakulima katika wilaya hiyo huku akisema kuwa muitikio wa wakulima katika wilaya yake ni mkubwa.

Amesema kuwa miche hiyo ya awamu ya kwanza itagawiwa katika vijiji vitatu kati ya vijiji 19 ambavyo wakulima wameonyesha nia na utayari wa kulima zao hillo.

Baadhi ya wakulima kutoka katika wilaya ya Butiama wamesema kuwa kutokana na elimu waliyopewa na wataalamu wa mkonge, zao hilo litakuwa zao kuu la biashara katika wilaya yao.

Magdalena Magira ameiomba bodi hiyo kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wakulima wengi kuanza kulima zao hilo katika wilaya hiyo kwa maelezo kuwa bado elimu haijawafikia wakulima wengi.

Mkulima wa zao hilo, Machage John amewataka wakulima wilayani Butiama kujitokeza na kutumia fursa ya kilimo cha zao hilo ili kuweza kuboresha maisha yao na kupambana na umasikini.

"Tumeambiwa zao hili linahimili ukame hivyo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, hili zao linatufaa niwaombe wakulima wenzangu wajitokeze hasa ikizingatiwa kuwa serikali inatoa bure miche ambayo pia inaletwa hadi huku vijijini bure kabisa" amesema John

Chanzo: www.mwananchi.co.tz