Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Dodoma watakiwa kuchangamkia soko la Ndugai

5c23f4eb680d521e47b58d97e0185c54 Wakazi Dodoma watakiwa kuchangamkia soko la Ndugai

Wed, 5 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka wakazi wa Dodoma kuchangamkia soko la kisasa la Ndugai kuuza bidhaa zao ili waweze kunufaika na fursa na mkoa huo kuwa makao makuu ya serikali na nchi.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Simbachawene ambaye ni mjumbe wa kikao hicho kutokana na kuwa Mbunge wa Kibakwe, wilaya ya Mpwapwa, alisema fursa hiyo ni adhimu kwa wakazi wa Dodoma hivyo wanatakiwa kuichangamkia kwa kuuza mazao yao kwa wingi katika soko hilo.

“Dodoma ni makao makuu ya nchi, makao makuu ya serikali, kidiplomasia Dodoma ndiyo Tanzania, hivyo wananchi wenzangu tunatakiwa kutumia fursa ya mji wetu kuwa makao makuu ya nchi kuchangamkia fursa zilizokuja nao mfano Soko na Ndugai,” alisema.

Simbachawene alisema wananchi wa mkoa huo wanatakiwa kulitumia soko hilo kuuza mazao yao ili wawaeze kupata fedha za kuendeleza maisha yao.

Alisema wananchi wa Dodoma wamekuwa wakisuasua kuchangamikia fursa ya uwapo wa soko hilo la kisasa ambalo linatumiwa na watu wengi wakiwemo watumishi wa serikali waliopo jijini hapa.

“Ninacho kiona ni kama wananchi wa Dodoma bado hao hawajaamua kulitumia soko hilo, hivyo halmashauri za mkoa za Bahi, Chamwino, Chemba, Kondoa, Mpwapwa, Kongwa na Jiji zinatakiwa kuwahamasisha kuichangamkia fursa hiyo kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kuuza bidhaa hizo wanazoazalisha katika soko hilo.

Pia aliwataka wananchi wa Dodoma kukaribisha wawekezaji na kushirikiana nao hasa wa sekta binafsi kwa kuwapa ardhi kwa ajili ili kukuza uchumi na kutengeneza ajira kwa vijana.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge akizungumzia umuhimu wa uwekezaji katika mkoa huo, alizitaka taasisi mbalimbali zinazohusika na miundimbinu wezeshi ya kurahisisha uwekezaji, kuandaa maeneo mapema kabla ya wawekezaji kwenda kuwekeza.

Alizitaka taasisi zinazohusika na miundombinu hiyo kama maji, umeme, barabara na huduma nyingine muhimu, kuandaa mazingira wezeshi katika maeneo ambayo yameandaliwa kupitia mpango kabambe wa jiji wa miaka 20 wa 2019-2039.

Chanzo: www.habarileo.co.tz