Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakandarasi wa umeme, Serikali waingia mgogoro wa kimikataba

Umeme Pic Wakandarasi wa umeme, Serikali waingia mgogoro wa kimikataba

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Mgogoro umeibuka katika utekelezaji wa mikataba ya miradi ya usambazaji umeme maeneo ya pembezoni chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) baada ya wakandarasi kudai haina zuio la uagizaji wa nguzo nje huku Serikali ikisimamia tamko la zuio la uingizaji wa nguzo nchini.

Baadhi ya wachambuzi walisema imefika wakati Serikali kufungia mikataba hiyo katika kifungu cha manunuzi ya vifaa vyote vinavyozalishwa hapa nchini, ili kuondoa mgogoro huo.

Msingi wa mgogoro huo unachagizwa na zuio la Aprili mwaka jana baada ya Waziri wa Nishati, January Makamba kuagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuingia zabuni za ununuzi wa nguzo kwa wakandarasi wanaokidhi vigezo ikiwemo kuhakikisha wazalishaji wadogo wa ndani wanapata soko.

Kauli hiyo ilikuwa inapigilia msumari na zuio la uagizaji wa vifaa vyote ikiwamo nguzo za umeme nje ya nchi baada ya Serikali kukubaliana na ombi la wazalishaji waliodai kuwa na uwezo wa kuzalisha nguzo ni mkubwa kuliko mahitaji ya Tanesco na REA katika miradi yake yote.

Wiki chache zilizopita, kampuni nne: OK Electrical and Electronics services Limited, Dieynem Limited, Derm Electrics Tanzania Limited na Central Electricals Int Limited zilisaini mikataba ya mradi wa kupeleka umeme katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa miji, awamu ya tatu, mzunguko wa pili.

Hata hivyo, wakandarasi hao walisema mikataba hiyo itakayogusa zaidi ya wateja 22,000 katika mikoa minane kwa thamani ya Sh76bilioni, haikuwa na kipengele kinachozuia uagizaji wa vifaa nje.

Kampuni ya OK Electrical and Electronics Services Limited iliyosaini mkataba wa miradi miwili Juni mwaka jana inatakiwa kukamilisha miradi hiyo Januari 5, mwaka ujao lakini imekamilisha mradi huo kwa asilimia 60 kutokana na changamoto ya uhaba wa nguzo.

“Hii ni tenda ya kimataifa ndio maana kulikuwa na kampuni kutoka Misri, Uganda, Kenya, China. Hakuna kipengele kinachozuia mkandarasi kuagiza nje ila imeacha free (haijasema kitu), sasa tutafuata tamko la Serikali lakini haitufungi kimkataba,” alisema Revocatus Mwankemwa, meneja miradi wa kampuni hiyo.

Mkurugenzi wa Ufundi wa kampuni ya Dieynem Limited, Novatus Lyimo alisema anahitaji nguzo zaidi ya 8,000 kutekeleza mradi wa kusambaza umeme pembezoni mwa mikoa ya Tanga na Tabora.

“Kwa sasa tunaandaa scope (taarifa ya mahitaji ya nguzo), sisi tutaangalia kama tutaona kuna uhaba, tutaagiza nje kwa sababu hizi zabuni hazikuwa na zuio la kuagiza vifaa nje,” alisema Lyimo.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy alisema; “kwa maslahi ya Taifa kwanini ukanunue nguzo nje wakati zinazalishwa ndani? Hata kama hatujafungia (kimkataba), hakuna atakayeruhusiwa kuingiza nguzo, labda alete kwa ajili ya kujengea mabanda ya kuku.”

Msingi wa kauli yake ulichagizwa na ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa kuhusu madai yasiyokuwa na ushahidi kuhusu uhaba wa nguzo za umeme katika baadhi ya miradi ya REA.

Awadhi Said Shedaffa aliyedai ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Viwanda vya Nguzo (Tawappa) alisema uzalishaji wa nguzo umefikia wastani wa milioni tatu kwa mwaka ikilinganishwa na mahitaji ya nguzo milioni moja kwa REA na Tanesco.

REA ilianza kutekeleza awamu ya kwanza kwa Sh80.5bilioni iliyowafikia wateja 37,713, awamu ya pili iliyoanza mwaka jana hadi Machi 2023 itaunganishia wateja wa awali 15,366 kwa bajeti ya Sh31.34bilioni na awamu hii ya tatu iliyozinduliwa wiki mbili zilizopita ni kwa wateja zaidi ya 22,000.

Chanzo: Mwananchi