Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakandarasi umeme pasua kichwa

UMEME Vunjwa Wakandarasi umeme pasua kichwa

Fri, 3 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pamoja na juhudi za serikali za kutaka kuwafikishia umeme wananchi wa vijijini kwa wakati kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), baadhi ya wakandarasi wamekuwa kikwazo kwa miradi hiyo.

Wabunge walisema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati wakichangia katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi alisema mradi wa Rea unatekelezwa kwenye vijiji 11 vya jimbo lake, lakini changamoto wanayokumbana nayo ni mkandarasi.

Alisema katika Kijiji cha Lugala mkandarasi hajafanya kitu chochote hata kuchimba mashimo bado na nguzo hazipo na kuiomba Wizara ya Nishati kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi huyo.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Maimuna Mtanda aliyesema wakandarasi wa Rea katika eneo lake walipewa kazi tangu Agosti, mwaka jana lakini wanachelewesha kazi kwa kisingizio kuwa vifaa vimepanda bei.

Alisema mkandarasi aliyeko Newala Vijijini alipewa kazi ya kuweka umeme katika majimbo ya Newala Vijijini, Newala Mjini, Tandahimba na Newala, lakini ufanyaji kazi wake haueleweki hivyo wamemchoka.

“Jimbo la Newala Vijijini, vijiji 33 tu kati ya 107 ndivyo vyenye umeme, mkandarasi mpaka ninavyoongea amefika kata mbili tu ambazo zina vijiji 11, hali ambayo inatia wasiwasi kwamba ikifika Desemba mwaka huu atakuwa amemaliza vijiji vyote 74 ambavyo havina umeme.”

“Kamati inayohusika na masuala ya nishati ilipokwenda kutembelea baadhi ya miradi, ikakuta katika eneo la Pwani mradi mmojawapo wa Rea umetekelezwa kwa asilimia 20 tu, sasa kama utekelezaji ni asilimia 20 kwenye Rea, hivi mnafikiria tunaweza kuendelea kwa jinsi gani,” alisema Mbunge wa Lulindi, Issa Mchungahela.

Mbunge wa Chemba (CCM), Mohamed Monni alisema mradi wa Rea unatekelezwa kwenye vijiji 50 katika jimbo lake, lakini mpaka sasa mkandarasi amewasha umeme kwenye kijiji kimoja tu ndani ya mwaka mmoja, hivyo itamchukua miaka 50 kuwasha umeme kwenye vijiji vyote.

Mbunge wa Makete, Festo Sanga alisema wizara hiyo inapaswa kuhakikisha wananchi walioweka nyaya kwenye makazi yao wanapata umeme haraka.

Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa alisema wizara hiyo inapaswa kujielekeza katika kusambaza umeme katika maeneo ya vijijini na kwenye vitongoji. Awali, wabunge walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka ruzuku ya Sh bilioni 100 kupunguza bei ya mafuta kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.

Walitoa pongezi hizo wakati wakichangia bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2022/2023. Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) alisema mafuta hayajashuka bei katika soko la kimataifa, lakini mamlaka ya Rais Samia imeshusha bei hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live