Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakala wa Vipimo awajia juu wauza nyama

Afdaed33d627caf358ade254891f8b6b.jpeg Wakala wa Vipimo awajia juu wauza nyama

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKALA wa Vipimo mkoa wa Kilimanjaro (WMA) imetoa onyo kwa baadhi ya wafanyabiashara wenye mabucha ya nyama kuacha tabia ya kuchezea mizani .

Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa wa Kilimanjaro Dennis Misango, aliyasema hayo jana wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi zake zilizopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Alikiri kuwepo kwa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi kuuziwa nyama pungufu na wafanyabiashara huku mezani zikiwa zimechezewa kwa lengo la kujipatia faida kubwa zaidi kwa haraka.

Alisema kumekuwapo na tabia ya makusudi kwa baadhi ya wafanyabiashara ya kuwaibia wateja wao na kwamba wakala wa vipimo mkoani hapa imejipanga kufanya oparesheni ya kuhakikisha wale wote ambao wanahusika na tabia hiyo watachukuliwa sheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.

"Nawaonya wafanyabiashara wa bucha za nyama ambao wamekuwa na tabia za makusudi za kujipatia fedha kwa njia ya kuwaibia wateja wao, kuacha tabia hiyo kwani tutakapo wabaini tutawakamata na tutawachukuliwa hatua kali za kisheria ,"alisema

Misango alisema kama ambavyo muongozo wa wakala wa vipimo unavyowataka wamejipanga kuhakikisha inafanya ukaguzi wa mara kwa mara na hata ule wa kustukizia ili kuwakamata wafanyabiashara wote wanaochezea mizani ili kuwaibia wananchi.

"WMA chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kufanya uhakiki wa mizani kabla ya kuuziwa nyama maana tabia hii ya wizi imekuwa ikishamiri,"alisema

Aidha, alisema lengo ni kuwawezesha wananchi kutambua mizani iliyosahihi inayoruhusiwa kwa biashara na ile iliyochezewa ambayo hairuhusiwi kwa biashara.

Nao, baadhi ya wananchi walisema wamekuwa wakiuziwa nyama pungufu kutokana na wafanyabishara kuchezea mizani ikiwemo kuweka sumaku chini ya mizani ili kuongeza uzito wa nyama.

"Mimi nafanyabishara ya chakula lakini nimejikuta nikipata hasara na kupoteza mtaji maana nimekuwa najua nikinunua nyama kilo tano najua naweza kuhudumia kiasi flani cha chakula lakini najikuta nyama imeisha na chakula hakijaisha,"alisema Aisha Miraji

Chanzo: www.habarileo.co.tz