Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakala wa Uvuvi waanzishwa kusaidia vijana

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali imeanzisha Wakala wa Uvuvi ili kuwapatia elimu vijana nchini kuhusu masuala ya uvuvi, lengo likiwa ni Taifa kunufaika na rasilimali zake.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 8, 2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akisema kuwa Serikali imeanzisha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri) ili kufanya tafiti na kuvumbua teknolojia zitakazosaidia kuleta tija katika uvuvi.

Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asha Mshimba Jecha aliyetaka kujua wananchi wa ukanda wa bahari na maeneo ya maziwa wameandaliwaje kufaidika na rasilimali zinazopatikana kwenye maeneo hayo.

Ulega amesema sekta ya uvuvi inasimamiwa na sera, sheria na miongozo iliyoandaliwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi na Taifa wananufaika na uvuvi.

"Sera ya uvuvi inaelekeza ushirikishwaji wa wananchi katika kusimamia rasilimali za uvuvi ambapo vimeanzishwa vikundi vya usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi," amesema Ulega.

Hata hivyo, amesema wizara hiyo imeanzisha dawati la sekta binafsi ili kuwasaidia wavuvi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz