Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakaguzi wa ngozi watakiwa kusaidia ubora wake

2e7a4f5cf6afade29934bc9658c20614 Wakaguzi wa ngozi watakiwa kusaidia ubora wake

Sat, 13 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKAGUZI wa Ngozi nchini wametakiwa kutambua kuwa uzalishaji mbovu wa zao la ngozi unachangia kurudisha nyuma viwanda vinavyotegemea zao hilo katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Wakaguzi hao wametakiwa kuhakikisha wanasimamia uzalishaji wa ngozi bora inayofaa kutumika katika uzalishaji wa bidhaa kwenye viwanda vilivyopo nchini.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole Gabriel alisema hayo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa pamoja na Tanzania kuwa na idadi kubwa ya mifugo, lakini bado zao la ngozi halifanyi vizuri.

“Nchi yetu ni ya pili kwa wingi wa mifugo katika Bara la Afrika, lakini pamoja na mafanikio hayo, zao la ngozi bado halifanyi vizuri, kujikwaa siyo kuanguka, tujipange upya kufufua sekta hii, tunahitaji kuongeza thamani stahiki katika mazo ya mifugo ambayo ni nyama, maziwa na ngozi,” alisema Profesa Gabriel.

Alisema kwa takwimu hadi kufika juzi, Tanzania ina ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, kondoo milioni 5.6 na nguruwe milioni mbili.

"Hii ni sekta inayokuwa kwa zaidi ya asilimia tano kwa mwaka na inachangia kwenya pato la taifa zaidi ya asilimia saba, kwa hiyo tunatakiwa kuhakikisha tunasimamia ng`ombe kuanzia kwa wachunaji kwa sababu ukishakosea kuanzia hapo ndio unaharibu ngozi, na namna inavyohifadhiwa ili hata wanaozinunua wapate faida… ombi langu ni kwamba tumedhamiria kuboresha sekta ya ngozi kwa kasi kubwa, tunatakiwa tupambane,” alisema.

Aidha, aliwataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kutekeleza waraka namba moja wa Rais wa mwaka 2002 kwamba asilimia 15 ya mapato irudishwe kuboresha sekta ya mifugo jambo litakalochangia kuwepo kwa mnyororo wa thamani wa zao la ngozi na kuleta tija katika uchumi wa nchi.

Alisema ni muhimu halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba asilimia 15 ya mapato yanayopatikana katika sekta hiyo inatumika katika kuhudumia sekta hiyo.

“Kwa kutekeleza hilo na kulisimamia kwa ufanisi naamini itasaidia kumaliza matatizo yote yaliyopo katika sekta hii ikiwamo masuala ya ngozi, matibabu, madawa na majosho. Ubora wa ngozi unashabihiana na afya ya mnyama, kwa muktadha huo tunahitaji kuwekeza pia katika chanjo, unyonyeshaji na malisho na ni wakati muafaka kanuni ya uogeshaji na ya chanjo nayo isimamiwe ipasavyo,” alisema Profesa Gabriel.

Kwa upande wake mtaalamu wa sekta ya ngozi Emmanuel Muyingi alisema tatizo kubwa linalochangia uzalishaji mbovu wa zao hilo ni uchunwaji mbovu wa ng’ombe kwenye machinjio kwenye machinjio, uandaaji na uhifadhi mbaya wa ngozi baada ya kuchinja na baadhi ya machinjio kuwatumia wachunaji wasio na taaluma hiyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz