Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali wazindua umoja kutafuta soko

Dom Wajasiriamali wazindua umoja kutafuta soko

Mon, 17 May 2021 Chanzo: ippmedia.com

Umoja huo unaojulikana kama ‘Kijiji kipya’ pia utawanufaisha na programu za mafunzo zitakazotolewa na serikali ya Korea Kusini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu wa umoja huo mkoani humo, Christopher Dioniz, alisema kuwa kijiji kipya ni mtandao wa pamoja na taasisi ya mama ya Saemoul Undong ya nchini Korea Kusini.

“Kwa hapa nchini kijiji kipya kinaundwa na vikundi jamii vya wajasiriamali vikiwamo vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambavyo vinapata mikopo ya asilimia 10, inayotengwa na serikali kupitia halmashauri zake,” alisema Dioniz.

Alisema umoja huo unalenga kukusanya watu na kuwaunganisha ili kuwa na nguvu ya pamoja na kujiletea maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na mazingira.

Katibu huyo alisema umoja huo utajenga ari ya wananchi kuwa na moyo wa kujiamini, kujituma, kujitolea na kushirikiana kwa lengo la kujiletea maendeleo na maisha bora na kushirikiana na serikali na asasi zingine za kiraia kitaifa na kimataifa.

“Pia kijiji kipya kitafanyika benki ya habari kwa wanakijiji (vikundi) ili kupata taarifa za masoko, kubadilishana uzoefu kati ya kikundi na kikundi na kuboresha utendaji wa vikundi kutokana na mafunzo mbalimbali yatokayotolewa ndani na nje ya nchi,” alisema Dioniz.

Alisema mpaka sasa umoja huo umefungua matawi yake katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Ruvuma, Morogoro na Dodoma na lengo ni kufika katika maeneo yote nchini.

Naye Mratibu wa Kijiji kipya nchini, Henry Mbwambo, alisema programu za mafunzo ambazo zitatolewa na Serikali ya Korea Kusini itahusisha wanavikundi pamoja na maofisa wa serikali.

Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo katika sekta za uzalishaji mali ili kukuza mitaji yao kama ambavyo vikundi vilivyopo nchini Korea Kusini vilivyopiga hatua.

“Dhana ya kijiji kipya inatokana na neno la Kikorea la ‘Saemoul Undong’ ikimaanisha kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kufikia mafanikio na kuachana na utegemezi,” alisema Mbwambo.

Akizindua umoja huo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, aliwataka kushirikiana ili kufikia malengo kwa kubadilishana uzoefu.

Chanzo: ippmedia.com