Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali wataka busara wakati wa utatuzi migogoro

Wajasiriamali Wajasiriamali wataka busara wakati wa utatuzi migogoro

Wed, 16 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Kwa muda mrefu kulikuwa na mgogoro baina ya wajasiliamali na serikali kutokana na wajasiliamali hao kufanyia kazi zao kwenye eneo ambalo usalama wake ni mdogo, hivyo serikali kuwataka waondoke huku wao wakigoma kwa madai ya kutotengewa eneo la kufanyia biashara zao.

Hivi karibuni, serikali ilitumia nguvu kuwaondoa wajasiliamali hao kwenye eneo hilo hali iliyozua vurugu kwa wajasiriamali hao kufunga barabara Kuu ya Tanzania na Malawi kwa kutumia mawe na meza walizokuwa wanafanyia biashara mpaka Jeshi la Polisi lilipoingilia kati.

Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe alifanya mkutano na viongozi wa wajasiriamali na kukubaliana kuwaacha waendelee na shughuli zao mpaka serikali itakapowatafutia eneo mbadala la kufanyia kazi zao.

Wakizungumza na Nipashe juzi, baadhi ya wajasiriamali hao walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakisumbuana na serikali kuhusu eneo hilo lakini hakuna mwafaka wa kudumu, hivyo wakawaomba watendaji wa serikali kuheshimu makubaliano ya sasa.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Esther Nyabula, alisema kabla ya kufikia makubaliano ya mwishoni mwa wiki, maofisa wa serikali wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuwashurutisha kuondoka bila kuwaonyesha eneo wanalotakiwa kufanyia shughuli zao.

Alikiri kuwa eneo hilo ni hatari kwa maisha yao lakini hawana namna kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu, hivyo akasisitiza kuwa wamekuwa makini wanapofanya kazi hizo na kwamba hakuna ajali iliyowadhuru.

“Tunamwomba mkurugenzi, manyanyaso tuliyokuwa tunapata yaishe. Hatuna mahali pengine ambapo tunaweza kwenda kuuzia matunda yetu zaidi ya hapa maana sisi wateja wetu hawa ni wasafiri wa kwenye magari,” alisema Nyabula.

Alisema hata kama wataondolewa basi wapelekwe eneo ambalo magari yatakuwa yanapita ili waendelee kufanya biashara wakiwa na uhakika wa wateja kuwafuata kama ilivyo kwenye eneo hilo.

Naye Rebecca Mwakamela alisema migogoro ya mara kwa mara imekuwa ikiwanyima uhuru wa kufanya shughuli zao na kwamba imekuwa ikiwatengenezea uhasama na viongozi wa serikali akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rungwe.

Alisema kabla ya kumaliza mgogoro huo, walikuwa wana hasira na kiongozi huyo lakini kutokana na busara aliyoitumia kumaliza mgogoro huo mara ya mwisho walimsamehe na hawana kinyongo tena.

Wakati wa kusuluhisha mgogoro huo, mkurugenzi huyo aliwataka wajasiliamali kuwa makini wanapoendelea na shughuli zao kwa maelezo kuwa katika eneo hilo wakati mwingine huwa kunakuwa na msongamano wa magari, hivyo kuwa na hatari ya kudhurika na kwamba ndio sababu ya serikali kutaka kuwaondoa.

“Kwa sasa mtaendelea na biashara zenu na sisi tutaendelea kuwatafutia eneo ambalo mtakuwa salama na mtafanya biashara zenu kwa uhuru, lakini pia muendelee kushiriki kwenye shughuli za maendeleo,” alisema mkurugenzi huyo.

Kiwira ni miongoni mwa maeneo ambayo maofisa wa Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS) wameweka vibao vinavyozuia wananchi kufanyia biashara lakini bado shughuli hizo zinaendelea.

Chanzo: ippmedia.com