Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali waomba Maonesho yaongezwe

5960e19f9d3f0710edf3713f41d4bf70 Wajasiriamali waomba Maonesho yaongezwe

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAJASIRIAMALI mbalimbali wanaoshiriki katika Maonesho ya Wakulima Nanenane, Kizimbani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wameiomba serikali kuongeza maonesho zaidi ili kutoa nafasi ya kuonesha bidhaa wanazozalisha na kupata soko zaidi kwa ajili ya kuongeza kipato.

Mjasiriamali Wache Makame Simai wa kijiji cha banda maji Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja anayetengeneza sabuni za aina mbalimbali kwa kutumia malighafi asilia alisema wamefurahishwa na kuwepo kwa maonesho hayo ambayo yametoa fursa kwa wajasiriamali kuonesha bidhaa mbali mbali wanazozizalisha.

Kwa mfano alisema yeye anatengeneza bidhaa za sabuni zinazotokana na malighafi ya Mkaratusi na majani yake kuyasaga na kupata unga ambao ni tiba ya ugonjwa wa mapele na kusafisha ngozi.

Alisema ni mara yake ya kwanza kushiriki katika maonesho hayo ambayo yamempa fursa kubwa ya kuonesha bidhaa zake na kuzitangaza katika soko.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria maonesho kama haya ambapo nimetengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni zinazotokana na malighafi ya Karafuu pamoja na Makonyo ambayo ni sehemu ya tiba kwa binadamu,” alisema.

Aidha, Time Kombo alisema ameanza kutengeneza unga wa mronge kwa matumizi ya chakula ukiwa ni lishe nzuri pamoja na tiba kwa maradhi mbali mbali ikiwemo kusaidia kuondosha gesi na usafishaji wa figo.

“Nimeanza kutengeneza unga wa mronge ambao unatokana na mboga ya majani ambayo hii ni mjarabu kwa kutibu maradhi mbali mbali ikiwemo kuondosha gesi na kusafisha figo na kushusha sukari mwilini,” alisema.

Ofisa Uwezeshaji wa Kiuchumi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Nairat Abdalla Ali akizungumza katika maonesho hayo alisema zaidi ya wajasiriamali 1,609 wamewezeshwa kiuchumi kupitia mradi wa WEZA 111 ambao lengo lake kubwa kuwapatia mafunzo mbali mbali wajasiriamali kufikiya malengo ya kujitegemea.

Alisema katika mradi wa WEZA 111 ambao unafadhiliwa na Milele Foundation umepata mafanikio makubwa kwa wajasiriamali kuweza kutengeneza na kuzalisha bidhaa za aina mbali mbali kuanzia za mikono ikiwemo kusuka mikoba ya ukili,pamoja na kutengeneza bidhaa sabuni za aina mbalimbali ikiwemo za maji na kuingia katika soko kwa mafanikio makubwa.

“Mradi wa kuwawezesha wajasiriamali kupiga hatua kubwa na kuondokana na umasikini WEZA 111 umepata mafanikio kwa kuwawezesha wanawake wengi vijijini kutengeneza bidhaa nyingi zikiwa na viwango na kuingia sokoni,” alisema.

Mratibu wa Milele foundation, Alice Mushi alisema wataendelea na mikakati yao ya kuwaunga mkono wajasiriamali katika kuzalisha bidhaa na kuingiza kipato.

“Malengo yetu ni kuwakomboa wanawake na umasikini kwa kuwapatia mbinu za ubunifu wa uzalishaji wa bidhaa mbali mbali na kuingiza kipato,” alisema.

Maonesho ya nane nane yaliyofanyika Kizimbani mkoa wa mjini Magharibi Unguja yamewashirikisha zaidi ya taasisi 120 ikiwemo wajasiriamali kutoka Unguja na Pemba.

Chanzo: habarileo.co.tz