Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali walalamikia sheria za viwanda zisizo rafiki

11093 WAJASRIAMAL+PIC TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya jitihada za Serikali za kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini, baadhi ya wajasiriamali wadogo wameeleza kuwa  sheria zinazosimamia masuala ya viwanda si rafiki kwao jambo ambalo linapunguza tija ya ukuaji wa viwanda.

Wakizungumza leo  Agosti 9 wakati wa Kongamano la 18 la viwanda vidogo na vya kati barani Afrika lililofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) wafanyabiashara hao wameeleza kuwa sheria nyingi hazimpi kipaumbele mjasiriamali mdogo hali inayoshusha kasi ya uwekezaji.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Cornwell Tanzania,Elizabeth Lema amesema sheria hizo bado hazijaleta tija hasa kwa wafanyabiashara wenye mitaji midogo huku akizitaka mamlaka husika kufanya maboresho yatakayo akisi mazingira halisi ya kitanzania.

“Sheria zetu bado zinahitaji mabadiliko,sheria zinatakiwa zitusaidie sisi wajasiriamali tuweze kukua kwa sababu nyingi zipo katika levo  ya juu sana na wengi hawazielewi,”amesema.

Pia amesema wajasiriamali wengi bado hawajazielewa sheria kutokana na kuwa zimeandikwa kwa lugha ya kigeni (Kiingereza) hivyo kuna haja ya kupewa elimu zaidi.

“Sheria nyingi zinawatazama wawekezaji walioendelea, kwa mfano mimi natengeza virutubisho na dawa asilia lakini naambiwa nifanye GMP (Good Manufacturing Practice) kitu ambacho ni kigumu,” amesema.

Naye, Neema Swai amesema moja ya changamoto inayowakabili kwa sasa ni hali ngumu ya biashara huku wakitakiwa kulipa kodi mbalimbali za Serikali hali inayowarudisha nyuma wafanyabiashara.

“Biashara imekuwa ngumu sana inafikia muda unshindwa hata kupata hela ya kodi za serikali kutokana na mzunguko kuwa mdogo,” amesema.

Mmiliki wa Kampuni ya Bagamoyo Harvest, Teddy Davis ameshauri Serikali kuandaa mkakati wa kuzinusuru bidhaa za ndani kwa kuweka asilimia 50 ya bidhaa za ndani katika masoko na maduka makubwa zikiwamo Supermarket.

Awali, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM, Profesa Boniventure Rutinwa amewataka wajasiriamali kuzitumia vyema tafiti zinazofanywa na wanataaluma nchini katika kuongeza tija ya uzalishaji nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz