Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali waitwa kusajili bidhaa

Tanzania Bureau Standards Tbs Quality Imports Wajasiriamali waitwa kusajili bidhaa

Thu, 9 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAJASIRIAMALI kote nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kusajili bidhaa zao na vipodozi katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na maeneo yao wanayozalishia bidhaa za vyakula na kabla ya muda wa miezi mitatu waliopewa kumalizika.

Wito huo ulitolewa jana na Ofisa Uhusiano Mkuu wa TBS, Rhoida Andusamile, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa.

Alisema TBS imekuwa likishiriki maonesho ya Sabasaba kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ambao wanatembelea maonesho hayo ili waweze kujua utaratibu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozizalisha na kwa walaji waweze kutambua bidhaa bora ni zipi na zisizo na kiwango ni zipi.

Kwa mujibu wa Andusamile, katika maonesho ya mwaka huu wamekuja na nguvu ya kuhamasisha wajasiriamali kuhakikisha wanasajili bidhaa zao, vipodozi pamoja na maeneo yao wanayozalishia bidhaa za vyakula.

Alifafanua kuwa mwaka jana, Sheria ya Fedha Namba 8 ya Mwaka 2019 iliipa TBS mamlaka ya kusajili bidhaa za chakula na vipodozi, jukumu ambalo awali lilikuwa linasimamiwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

"Kwa hiyo tangu Julai Mosi mwaka jana tumekuwa tukifanya kazi hii ya kusajili maeneo ya uzalishaji, maeneo ya kuhifadhia vyakula na vipodozi na vile vile kuthibitisha ubora wa bidhaa kazi ambayo tulikuwa tukiifanya tangu awali," alisema Andusamile.

Alisema wanatumia fursa ya kushiriki kwao maonyesho ya Sabasaba kuwahamasisha zaidi wajasirimali kujitokeza kwa wingi kujisajili kwani bado wanasuasua.

"Na tumeshatoa tangazo hivi karibuni kuwataka wasajili hizo bidhaa za vyakula na vipodozi, lakini bado wengi wanajivuta vuta,” alisema.

Alisema wajasiriamali waje wasajili na sasa hivi wanaweza kujisajili kwa njia ya mtandao kama wamekwama basi wafike ofisi za TBS ili wapate msaada.

Aliongeza kwamba kwa sasa wametoa muda wa miezi mitatu ili waweze kufanya hivyo na iwapo muda huo utamalizika, shirika la viwango wataanza kuwatembelea katika maeneo yao ya biashara.

"Tukiona hawajatekeleza maagizo haya basi hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao, tunawasihi sana huo muda wa miezi mitatu waliopewa unaisha mwezi huu wa Julai mwishoni hivyo kuanzia Agosti tutaanza kuwakagua,” alisema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live