Mwenyekiti wa umoja huo, Haruna Kifimbo, alisema hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonyesho hayo.
Kifimbo alisema maonyesho hayo yanatarajiwa kushirikisha zaidi ya wajasiriamali 700, ambao wataleta na kuonyesha bidhaa zao mbalimbali kutoka maeneo yote nchini.
“Kutokana na serikali kufuta maonyesho ya Nanenae mwaka huu sisi kama wajasiriamali tumeona siku hizi zisipite bure, hivyo tumeandaa maonyesho haya ambayo yatahusisha watu mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali ya nchi,” alisema Kifimbo.
Aidha, alisema kuwa maonyesho hayo yatafanyika kuanzia Agosti 1, hadi 13, ambapo pamoja na wajasiriamali makundi mengine kama Wizara ya Maliasili na Utalii watakuwapo pia kuonyesha shughuli zao.
Kadhalika, Kifimbo alisema maonyesho hayo ni fursa kwa wajasiriamali nchini wakiwamo wa Jiji la Dodoma kutangaza bidhaa wanazozalisha na kuongeza wigo wa masoko.
Vilevile, alisema kuwa mkoa tayari umeshawapatia barua ya kuruhusu wao kufanya maonyesho hayo ya wajasiriamali katika muda huo.
Mapema mwaka huu Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, ilitanga kufuta maonyesho ya Nanenae.
Waziri Mkenda alisema sababu kubwa ni kuitumia fedha ambazo zingetumika katika maonyesho hayo ili kuimarisha shughuli za ugani na kuongeza tija kwenye kilimo.