Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali wa kilimo kupata mikopo kidigitali

Fedhapic Wajasiriamali wa kilimo kupata mikopo kidigitali

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika jitihada za kuinua sekta ya kilimo nchini, taasisi ya fedha ya Victoria Finance kwa kushirikiana na Pass Trust, inatoa mikopo kwa wajasiriamali wa kilimo kwa njia ya kidijitali kupitia lengo likiwa ni kutoa huduma ya mitaji kwa wajasiriamali hao.

Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari leo jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Victoria Finance, Julius Mcharo amesema taasisi hiyo imeanzisha huduma hii ya kidijitali ili kukidhi mahitaji ya mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, ikiwa ni pamoja na wale wanaojihusisha na biashara za mazao ya kilimo na mifugo.

"Kwa kutambua changamoto wanazokabiliana nazo wajasiriamali hawa, taasisi yetu imeanzisha aina mbalimbali za mikopo ya muda mfupi ili kuimarisha biashara zao kwa ufanisi, urahisi na kwa uhakika zaidi," amesema Mcharo.

Mcharo amesema akizungumza dhamira yao ni kutoa mitaji kwa wajasiriamali wa kilimo itakayosaidia kustawi kwa sekta ya kilimo na kwamba mikopo hiyo imeundwa kwa kusudi la kusaidia gharama za mavuno, usindikaji na maghala ili wajasiriamali waweze kunufaika zaidi katika shughuli zao.

"Wajasiriamali wanaweza kupata mikopo kuanzia Sh100,000 hadi 1,000,000 kwa mtu binafsi au kikundi kulingana na mahitaji yao. Pia kiasi hiki cha mkopo kinaweza kutolewa kwa njia ya simu ya muombaji, ili kurahisisha malipo ya fedha kwa wakati na wakati huohuo kurahisisha urejeshwaji wake kwa wakati," amesema Mcharo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Pass Trust, Yohane Kaduma amesema wanafahamu kwamba sekta ya kilimo ndiyo nguzo ya uchumi wa nchi hivyo ushirikiano wao na Victoria Finance ni juhudi za kusaidia sekta hiyo.

"Sisi tunatoa dhamana za mikopo ya kidijitali kupitia simu za mkononi, kuruhusu wakulima kupata huduma ya mikopo kutoka kwa taasisi za kifedha tukianza na Victoria Finance," amesema.

Pia ameongeza kuwa ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya kuwawezesha wajasiriamali wa kilimo, kukuza mnyororo wa thamani wa kilimo na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live