Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali Iringa kuuza mbegu za maboga Rwanda

8d6de9d189a3d26224f7e47b2e185233 Wajasiriamali Iringa kuuza mbegu za maboga Rwanda

Tue, 1 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wajasiriamali mkoani Iringa wamepata soko la mbegu za maboga nchini Rwanda baada ya kushiriki Maonesho ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) maarufu ‘Juakali’.

Kwa awamu ya kwanza, wafanyabiashara hao watasafirisha tani mbili za mbegu hizo na kiasi hicho kitakuwa kikiongezeka kila baada ya muda kwa kadiri ya mahitaji.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati Afrika Mashariki, Josephat Rweyemamu amesema hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa waliyopata wajasiriamali wa Tanzania katika maonesho hayo.

Kwa mujibu wa Rweyemamu, wajasiriamali hao watatafuta mbegu na kuzisaga kisha kuuza nchini Rwanda. Unga wa mbegu hizo hutumika kwa wingi kuchanganya katika chakula ili kuongeza virutubisho katika vyakula au vinywaji kadhaa.

“Kwa sasa wanaendelea na taratibu za kupata vibali ili kusafirisha mzigo wa kwanza kwenda Rwanda ambao ni tani mbili za unga huo wa mbegu za maboga,” alisema Rweyemamu na kuongeza kuwa, hatua hiyo itawaongezea kipato na kuimarisha ustawi wa wanakikundi.

Alisema mbali na kupata soko la bidhaa hizo nchini Rwanda, katika maonesho hayo Watanzania pia walifanikiwa kupata masoko ya bidhaa mbalimbali katika nchi za Kenya, Uganda na Sudan Kusini kutokana na ubora wa bidhaa zao.

Maonesho hayo ya hivi karibuni ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) maarufu ‘Juakali’ au ‘Nguvukazi’, yalifanyika Mwanza (Tanzania) na kukutanisha wajasiriamali zaidi ya 1,500.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live