Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahitimu 40 vyuo vikuu kunolewa kuziba pengo wataalamu sekta ya madini

Madini Pic Data Wahitimu 40 vyuo vikuu kunolewa kuziba pengo wataalamu sekta ya madini

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imezindua mafunzo tarajali kwa wanafunzi 40 waliohitimu vyuo mbalimbali nchini.

Mafunzo hayo yanayotolewa kwa muda wa mwaka mmoja (2024/2025) kwa wahitimu wasiokuwa na ajira, yatahusisha programu mbalimbali ikiwemo za uanagenzi, mafundi mchundo, wataalamu wa masuala ya madini ya fani nyingine zilizoanzishwa kukuza ujuzi wa vijana wa Kitanzania.

Akizungumzia mafunzo hayo hivi karibuni, Makamu Rais Mwandamizi - Kitengo cha Biashara Afrika, Terry Strong amesema mpango wa mafunzo hayo huwapa wahitimu wasio na ajira nafasi ya kupata uzoefu wa kazi ambao unakamilisha masomo yao, na unaweza kuwasaidia kushindana katika soko la ajira

Terry amesema mpango huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2009, umenufaisha jumla ya wahitimu 258 (pamoja na waliopo sasa) kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini Tanzania.

Pia, amewakaribisha wahitimu 10 wa mafunzo hayo kwa mwaka jana ambao wamepatiwa ajira za kudumu ndani ya kampuni hiyo.

Amesema walengwa ni asilimia 41 ya wanawake na asilimia 59 ya wahitimu wa kiume. Kati ya wahitimu 258 walioandikishwa, asilimia 34 ambao ni (87) waliajiriwa na GGML kwa mkataba wa kudumu katika nafasi mbalimbali, huku wengine wakiajiriwa kwa mkataba wa muda.

“Kwa kuzingatia mafanikio kadhaa yaliyofikiwa hadi sasa, GGML imejitolea kuendelea na mpango wa mafunzo kazini,” amesema.

Amesema mpango huo umetumika kama chanzo kikuu cha wahitimu kuing’arisha kampuni hiyo kwa vipaji walivyojaliwa na kuwatayarisha kutekeleza majukumu muhimu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela mbali na kuishukuru GGML kwa kutekeleza mpango huo alilipongeza kundi hilo la wahitimu wa vyuo mbalimbali waliobahatika kupata mafunzo GGML kwa mwaka huu 2024/2025.

“Kitendo cha kupata fursa hii ndani ya GGML, sio njia tu ya kupata uzoefu, lakini ni chachu ya kutambua uwezo wako kwa ukamilifu. Kabiliana na changamoto, tumia maarifa yako na uruhusu shauku yako ikupeleke kwenye ubora,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Ujuzi wa kampuni hiyo, Albert Rukeisa amesema, “sanjari na hilo nipende kutoa rai kwa vijana hawa, waswahili wanasema “Ukishikwa shikamana” Nendeni mkaweke bidii ya kazi, uaminifu, mkizingatia usalama na taratibu zote za mgodi nanyi mtayaona mema ya utii katika kujifunza kazi,” amesema.

Mmoja wa wanafunzi waliohitimu mafunzo hayo mwaka jana na kupata bahati ya kuajiriwa ndani ya GGML, Diana Laswai, mbali na kuishukuru kampuni hiyo waliishukuru Serikali kwa kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kutoa mafunzo kazini kwa vitendo.

Naye Grace Msafiri ambaye ni mmoja wa wanafunzi waliopata fursa ya mafunzo hayo mwaka huu, aliahidi kutumia kama nyenzo ya kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia usalama mahali pa kazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live