Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafugaji wazururaji kubanwa kisheria

Mifugo DPP Wafugaji wazururaji kubanwa kisheria

Sun, 3 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameziagiza halmashauri za wilaya kuboresha sheria ndogo ili ziweze kuwabana wafugaji wanaopitisha mifugo yao barabarani na kuigharimu Serikali kutumia fedha nyingi kufanya matengenezo.

Sendiga ameoa agizo hilo leo Desemba 2 mjini Babati, katika kikao cha Bdi ya Barabara wakati akizungumza na wajumbe wa bodi ya barabara ya mkoa huo.

"Halmashauri zote za wilaya zilizopo Manyara, nendeni mboreshe sheria ndogo na kuendelea kutoa elimu ya matumizi ya barabara ili tuokoe barabara zetu maana tunatumia fedha nyingi kuzifanyia matengenezo," amesema Sendiga.

Amesema wakurugenzi na Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) wakianza kusimamia sheria ndogo viongozi wa kisiasa wanyamaze wasiwatetee wafugaji.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuhusu ahadi za viongozi sekta zote zipeleke mpango kazi ofisini kwake kuonesha namna ya kwenda kutekeleza ahadi hizo.

"Ni lazima ahadi za viongozi zitekelezwe na madaraja makongwe ni vizuri kuyaangalia namna ya kuyatengeneza," ameeleza.

Awali akiwasilisha taarifa yake katika mkutano huo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Manyara, Dutu Masele amesema wameshafanya uthamini kwa wananchi wanaotakiwa kulipwa Sh9 bilioni za fidia kulipisha ujenzi wa barabara ya mchepuko.

"Tumeishawasilisha wizarani ombi la kulipa fidia barabara ya mchepuko ya kilometa 25," amesema Masele.

Meneja huyo ametaja vikwazo ambavyo wanakabiliana navyo kuwa ni mfumo wa manunuzi kuchelewa, mifugo kutembezwa barabarani, ufinyu wa bajeti na kutupa taka kwenye mitaro.

Naye Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema endapo hawatawapa kazi wakandarasi wazawa hawatainuka kiuchumi badala yake wakandarasi wa kigeni ndiyo wataendelea kunufaika.

Sendeka ameiomba Tanroads kuwashirikisha wabunge kwenye kazi wanazofanya kabla hawajaanza.

Kaimu meneja wa Tarura mkoani Manyara, Edwin Magiri akitoa taarifa yake amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo ipo asilimia 65 na mikataba 74 ya ujenzi wa barabara imeishasainiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live