Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafugaji 100,000 kunufaika mradi wa maziwa wa Tsh. bilioni 56

MAZIWA Bil 56/- mradi wa maziwa kunufaisha wafugaji 100,000

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ihakikishe fedha za mikopo kwa ajili ya sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi zinatolewa kwa wakati, kwa riba na masharti nafuu.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mradi wa ushirikiano wa wasindikaji na wazalishaji katika tasnia ya maziwa (TI3P).

“Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 40 na wenzetu ambao ni wafadhili wetu wa taasisi ya Bill na Melinda Gates wametoa dola milioni saba (Sh bil 16.2) ambapo tumeshuhudia utiwaji wa sahihi wa fedha hizi, ni matumaini yangu mradi huu utaongeza tija katika uzalishaji na ukusanyaji wa maziwa katika mfumo rasmi na kukuza uwezo wa viwanda vyetu katika uchakataji,” alisema.

Mtendaji Mkuu wa TADB, Frank Nyabundege alisema mradi huo wa miaka mitatu unalenga kuwafikia wafugaji 100,000 na viwanda kati ya 9 hadi 12 vitakavyosaidiwa kuandaa mikakati ya kibiashara na masoko.

“Katika sekta hii ya maziwa benki imewekeza zaidi ya bilioni 16.4 na kati ya fedha hizi tuliwakopesha moja kwa moja wafugaji na viwanda vya maziwa bilioni 15.6 ambazo bilioni 14 tulikopesha viwanda sita vya uchakataji na uzalishaji wa maziwa, milioni 546 vyama vya ushirika sita na milioni 706 tumekopesha kampuni na wafanyabiashara wadogo wadogo wanajishuhulisha na ufugaji,” alisema.

Majaliwa alisema mradi huo utakuwa chachu katika kukuza na kuongeza tija ya uzalishaji wa sekta ndogo ya maziwa.

Aidha, Majaliwa alisema sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji ni muhimu katika uchumi wa taifa licha ya kukabiliwa na changamoto ikiwemo sekta ndogo ya maziwa kutokana na jamii kutokuwa na elimu ya ufugaji bora wa kitaalamu.

Aidha, alisema ni wajibu wa TADB kuhakikisha inatoa mikopo hiyo kwa walengwa kwa muda mwafaka ili kusaidia kutatua changamoto.

Mwakilishi wa taasisi ya Bill na Melinda Gates, Marcella McClatchey alisema taasisi hiyo imetoa msaada wa Dola za Marekani milioni saba ili kuimarisha sekta ndogo ya maziwa nchini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live