Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi wapya 16 wa kujitolea wa Peace Corps waapishwa

Corpsss.jpeg Wafanyakazi wapya 16 wa kujitolea wa Peace Corps waapishwa

Thu, 11 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Leo, katika hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya Peace Corps Tanzania, Wamarekani 16 wameapishwa kuwa Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps.

Hafla hiyo iliongozwa na Balozi Michael Battle na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Dr Edith Rwiza, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania Stephanie Joseph de Goes.

Wafanyakazi wa kujitolea 16 walioapishwa leo ni kundi la kwanza la wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps kuhudumu nchini Tanzania toka kuanza kwa janga la UVIKO-19 hapo Machi 2020 ambalo lililosababisha kurudishwa nyumbani kwa zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 7,000 kutoka duniani kote ikiwemo 158 kutoka Tanzania.

Kwa wiki 12 zilizopita, wafanyakazi hawa wapya wa kujitolea wamekuwa wakipata mafunzo ya kina ya utamaduni wa Kitanzania, lugha ya Kiswahili na ujuzi mahsusi kulingana na sekta watakazozitumikia.

Baada ya kula kiapo, wafanyakazi hawa watakwenda kufanya kazi na kuishi na jamii za Kitanzania katikamikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Zanzibar ambako watahudumu kwa miezi 24 wakizisaidia jamiikushughulikia vipaumbele muhimu vya maendeleo, ikiwa ni pamoja na elimu, afya ya jamii na kilimo endelevu.

Katika hotuba yake, Dk. Rwiza aliielezea Programu ya Peace Corps kama kielelezo cha uhusiano wa karibu kati ya Marekani na Tanzania na kama urithi wa urafiki kati ya Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Marekani John Kennedy, ambaye ndiye muasisi wa Peace Corps.

Alitoa wito kwa wadau wote katika maeneo ambapo wafanyakazi hawa wa kujitolea watahudumu kuwapa msaada wa hali na mali ili kuwasaidia kushamiri katika utendaji kazi wao.

Akihutubia kabla ya kusimamia kiapo kwa wafanyakazi wapya wa kujitolea, Balozi Battle aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa wap ndio watakuwa sura ya Marekani kwa watu wengi watakaokutana nao. “Watu watawakumbuka ninyi, kwa sababu mlitembea miongoni mwao, mlifundisha na kujifunza pamoja nao ninyi mnawakilisha kile kilicho bora kabisa kuhusu Marekani, na mna fursa ya kuishi na kujionea kile kilicho bora kabisa kuhusu Tanzania.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Tanzania Country Stephanie Joseph de Goes alitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania, Chuo cha Ualimu Korogwe na familia zilizoishi na wafanyakazi wa kujitolea kwa kuisaidia Peace Corps kuwapokea na kutoa mafunzo ya Kiswahili na utamaduni wa Kitanzania kwa wafanyakazi wapya wa kujitolea kwa mafanikio makubwa.

Alisisitiza dhamira ya dhati ya Peace Corps kufanya kazi na Tanzania kwa moyo wa ushirikiano, unyenyekevu na heshima.

Kuhusu Peace Corps: Peace Corps ni mtandao kimataifa wa wafanyakazi wa kujitolea, wanajamii, wabia wa nchi zinazowapokea wafanyakazi hao na wafanyakazi wanaosukumwa na dhima ya shirika ya kuwa na dunia yenye amani na urafiki.

Kwa mwaliko wa serikali mbalimbali duniani kote, wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps hufanya kazi na wanajamii wa jamii husika katika miradi yao ya kipaumbele katika maeneo ya elimu, afya, mazingira, kilimo, maendeleo ya kiuchumi ya jamii na maendeleo ya vijana.

Kupitia huduma hii, wafanyakazi wa kujitolea na wale wote walio katika mtandao wa Peace Corps hujenga stadi mbalimbali wanazoweza kuzitumia mahali pengine na ujuzi wa kufanya kazi na watu wa tamaduni tofauti tofauti hivyo kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuwa kizazi kijacho cha viongozi wa kimataifa.

Toka Rais John F. Kennedy alipoanzisha Peace Corps mwaka 1961, zaidi ya Wamarekani 240,000 wamehudumu katika nchi 142 duniani kote.

Zaidi ya Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corpos 3200 wamehudumu nchini Tanzania toka programu hii ilipoanza mwaka 1961, wakifanya kazi katika sekta za elimu, kilimo na afya wakishughulikia vipaumbele muhimu vya maendeleo na wakati huo huo wakikuza amani na urafiki duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live