Serikali imesema wafanyakazi 279 waliokuwa wakifanya kazi na Kampuni ya Uendelezaji na Uendeshaji Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro (KADCO) wataendelea kupata stahiki zao kama kawaida serikalini.
Novemba 10, KADCO ilikabidhi rasmi kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kwa mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA).
Hatua hiyo ilikuja kufuatia tamko la Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alilolitoa Novemba 9 mwaka huu bungeni jijini Dodoma kufuatia mvutano uliodumu kwa mwaka mzima huku wabunge wakitaka TAA ichukue majukumu ya KADCO.
Akizungumza na wafanyakazi hao leo Jumatatu Novemba 13, 2023 katika ofisi za uwanja wa KIA, Profesa Mbarawa amesema hakuna mfanyakazi hata mmoja atakayepoteza ajira yake na Serikali itahakikisha wanaendelea kupata maslahi yao kama kawaida pamoja na kufanya maboresho makubwa katika kiwanja hicho.
"Naomba niwahakikishie wote ninyi na familia zenu mpo salama, kila mmoja yupo hapa kwa ajili ya kufanya kazi na kutafuta maslahi yake, mmeaga nyumbani mnakuja kazini na mnatamani na serikali inatamani mfanye kazi kwa mujibu wa sheria,"amesema Profesa Mbarawa
"Tunaenda kufanya mabadiliko makubwa katika kiwanja hiki, kiwanja cha ndege ni watu, bila ninyi hakiwezi kujiendesha chenyewe, ndio maana nikasema nije niongee na ninyi, huu ni uwanja wenu ni maisha yenu, hivyo tukaona sisi sote tuje kuongea na ninyi tuwahakikishie kwanza mko salama, mikono salama, na ajira zenu zipo salama,"
"Hakuna mtu yeyote ambaye atapoteza kazi yake, ajira na stahiki yake hata mmoja, kwa hiyo watu wasiwe na wasiwasi, twendeni tukafanye kazi kwa maslahi ya uwanja huu wa ndege, "amesema Profesa Mbarawa
Amesema Serikali itaweka miundombinu ya kisasa katika kiwanja hicho, ili kiweze kufanya vizuri zaidi na kwamba Serikali itaweka terminal ya kisasa pamoja na kuongeza ukubwa wa uwanja kwa maslahi mapana ya nchi.
"Kiwanja hiki kama tutajipanga vizuri tutaweka miundo mbinu ya kisasa na kikaweza kfanya vizuri kuliko hata kiwanja cha Dar es salaam, tukijipanga vizuri tunaweza kuwa na jengo la kisasa la uwanja wa ndege (terminal) la kisasa na tukaweza kuongeza uwanja ukawa mkubwa zaidi na tukaweza kutatua changamoto hizi ndogondogo zote,"
Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania(TAA), Musa Mburah, amesema wataendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida na kwamba ni jukumu lao la msingi kusimamia viwanja hivyo na kwamba KIA inaenda kuwa ni kiwanja cha ndege cha 59 kusimamiwa na TAA.
"Sisi kama mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania, tumekuja hapa kupokea maelekezo ya Waziri na kuendelea kutekeleza majukumu ya uendeshaji wa majukumu ya kiwanja hiki cha ndege cha KIA, tumepokea hili jukumu na tuko tayari kutekeleza na ni majukumu yetu ya msingi,"amesema Mburah
Naye, Mwenyekiti wa wa wafanyakazi wa uwanja huo, Juma Kimwaga ameishukuru Serikali na kusema mabadiliko hayo wameyapokea vizuri bila mashaka yoyote na wapo tayari kufanya kazi kwa kuwa wanaamini wapo mikono salama ya Serikali.
"Sisi ni watumishi wa umma, tumesikia sauti yako leo kwamba tuko salama, tukuhakikishie mheshimiwa Waziri sisi tupo tayari kufanya kazi popote na wakati wowote bila kujali, tumepokea mabadiliko haya vizuri bila mashaka yoyote kwasababu ya maelekezo ya serikali,"amesema Kimwaga