Wafanyabiashara wadogo, wakati na wajasiriamali wameshauriwa kutembelea banda la Mfuko wa Self lililopo katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Saba Saba ili kujifunza namna ya kupata mikopo itakayowawezesha kuboresha kazi zao.
Mfuko wa Salfie unajihusisha na mikopo kwa ajili ya wafanyakazi wa taasisi za serikali ambao wanataka kuboresha makazi yao, wakulima na Wazabuni katika Kampuni binafsi za aina mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko na Uhamashishaji Mfuko wa Self, Linda Mshana amesema ni wakati muhimu wa kuongeza Uwekezaji katika nchi hivyo wajasiriamali wenye vikundi, na wale wenye namba ya utambulisho ya mlipa Kodi (TIN NUMBER) wanakaribishwa.
"Tupo hapa ndani ya banda la Wizara ya Fedha na mipango tukitoa huduma mbalimbali kwa ajili ya wananchi tunawakaribisha kuja kutembelea banda letu ambapo wanaweza kupata fursa ambazo tunazitoa katika mfuko huu, tuna mikopo ya aina mbalimbali kwa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa," amesema Mshana.
Aidha, amewataka wananchi watakapopata nafasi ya kufika katika banda hilo wachukue fursa ya kuuliza maswali yote waliyonayo na kwamba riba zao ni nafuu hakuna mtanzania atakaye shindwa kupata mkopo huo kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.