Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wazalendo wamkuna Balozi Iddi

BALO Wafanyabiashara wazalendo wamkuna Balozi Iddi

Mon, 18 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema mchango mkubwa wanaoendelea kutolewa na wafanyabiashara wazalendo nchini utabakia kuwa ukumbusho kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo jana, wakati akipokea msaada wa vifaa mbali mbali kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar vilivyotolewa na Mwenyekiti wa kampuni za ZAT na Royal Group, Mohamed Raza Hassanali.

Raza ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, alikabidhi barakoa 400 kwa wananchi wa jimbo hilo pamoja na vyakula kwa ajili ya familia 218 zilizokumbwa na maafa kutokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni.

Balozi Iddi alisema wananchi wengi wanafarijika kutokana uamuzi wa wafanyabiashara wazalendo wanaounga mkono matatizo na majanga yanayowakumba katika maeneo yao.

Aidha, alipongeza kampuni hizo kwa jitihada zinazochukuliwa kuwa karibu na wananchi sambamba na Serikali katika kuona ustawi wa Jamii unaendelea kubakia salama na furaha licha ya changamoto zinazojitokeza.

Akizungumzia athari ya mafuriko ya mvua za masika za mwaka huu, Balozi Iddi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, aliwatahadhari wananchi kuendelea kuepuka kujenga makazi yao ya kudumu katika maeneo hatarishi.

Alisema maeneo ya kilimo, sehemu za mabwawa, mito pamoja na misingi ya maji ya mvua ni vyema zikaepukwa mapema ili kujihakikishia usalama wa maisha yao sambamba na hasara kubwa inayoweza kuleta usumbufu wa mchanganyiko wa mawazo yasiyokwisha ndani ya maisha yao.

Naye, Mohamed Raza Hassanali, alisema uongozi wa taasisi hizo umefikia hatua ya kutoa msaada huo kufuatia changamoto mbali mbali zinazowakumba watu wenye mahitaji maalum.

Akitoa shukrani kwa niaba ya uongozi, watendaji wa idara ya watu wenye ulemavu pamoja na watu wenye mahitaji maalum, Ofisa Jinsia Maendeleo wa Idara hiyo, Foum Shaaban, alisema milango bado iko wazi kwa mtu au taasisi yoyote ndani na nje ya nchi kusaidia kundi hilo la watu wenye mahitaji maalum.

Foum alisema msaada huo wa baiskeli za walemavu, vyarahani pamoja na fimbo maalum za kuwaongoza watu wasioona zitagaiwa kwa wahusika Unguja na Pemba kwa mujibu wa taratibu zilivyopangwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live